Mwanamke auawa kikatili Shinyanga, mumewe asakwa

Shinyanga. Sintofahamu imetawala katika Kijiji cha Songambele, Kata ya Salawe mkoani Shinyanga kufuatia kifo cha mwanamke aliyekutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili.

Marehemu ametambuliwa kuwa ni Mariam Mafumba (40), ambaye inadaiwa alikutwa amekufa asubuhi ya Machi 23, 2026, huku mwili wake ukiwa na dalili za kupigwa kwa kitu kizito, hali iliyozua hofu na maswali miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele, Razaro Enock amesema mauaji hayo yalitokea katika Kitongoji cha Machongo, na kwamba mazingira halisi ya kifo hicho bado hayajabainika.

Hata hivyo, amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa marehemu alikuwa na mgogoro wa kifamilia na mume wake, ambaye ametoweka na hajulikani alipo.

Kwa mujibu wa taarifa za wananchi, marehemu alikuwa akikabiliwa na changamoto katika ndoa yake, ikiwamo mume wake kutokuwepo nyumbani kwa muda mrefu.

Aidha, imeelezwa kuwa aliwahi kuishi na mwanaume mwingine aliyemtambulisha kama ndugu, lakini baadaye kubainika kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Inaelezwa kuwa mwanaume huyo aliondoka ghafla akiwa amechukua mali zake baada ya kutofautiana na mkewe na muda mfupi baadaye ndipo tukio hilo la kusikitisha lilibainika, jambo linaloendelea kuchunguzwa ili kubaini ukweli wake.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Janeth Magomi amesema uchunguzi wa awali unaonyesha marehemu alipigwa kwa kitu kizito sehemu mbalimbali za mwili, ikiwamo kichwani.

Amesema mtuhumiwa anahisiwa kuwa ni mume wa marehemu, Manyanda Mbuye ambaye ametoroka baada ya tukio hilo na anatafutwa na Jeshi la Polisi.

Kamanda Magomi ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ili sheria ichukue mkondo wake.

“Uchunguzi wa awali umebaini, chanzo kinachodhaniwa cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, ambapo mtuhumiwa alimshuku marehemu kuwa na uhusiano na mwanaume mwingine.”

Amesisitiza kuwa vitendo vya ukatili havikubaliki katika jamii, akiwataka wanandoa na familia kwa ujumla kutatua migogoro yao kwa njia ya mazungumzo badala ya kutumia nguvu.