Arusha. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametoa onyo kali kwa viongozi wa umma wanaoshindwa kusikiliza na kutatua kero za wananchi, akisema zama za viongozi wanaogeuza ofisi za umma kuwa kama mali binafsi zimepitwa na wakati.
Amesema viongozi wanaokerwa na malalamiko ya wananchi hawapaswi kuendelea kushika nafasi za uongozi, akisisitiza kuwa jukumu la kusikiliza na kutatua kero za wananchi halina mbadala.
Dk Nchemba ameyasema hayo leo Jumatano Machi 25, 2026 jijini Arusha wakati akizungumza katika mkutano wa 110 wa wadau wa elimu kwa umma ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Amesema Serikali haitavumilia kuona wananchi wanyonge wakinyanyaswa au kunyimwa haki zao kutokana na uzembe au dharau za baadhi ya viongozi.
“Kama wapo viongozi wanaona kushughulikia kero za wananchi kunawakera, tutawaomba waachie hizo nafasi haraka. Ofisi ya umma siyo duka lako binafsi,” amesema Dk Mwigulu.
Washiriki wa mkutano wa 110 wa Wadau wa Elimu kwa Umma ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)jijini Arusha leo. Picha na Filbert Rweyemamu
Ameongeza kuwa katika kipindi chake cha uongozi ataendelea kusimamia haki za wananchi, akisisitiza kuwa kusikiliza matatizo yao ni sehemu ya wajibu wa kiongozi kwa jamii.
Aidha, amewataka viongozi kutodharau kero za wananchi kwa kuziona ni ndogo, akisema kwa wananchi zinazowakabili ni kubwa na zinahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Katika hotuba yake, pia amezungumzia utendaji wa TBC, akisisitiza kuwa chombo hicho kinapaswa kukua na kuendana na hadhi na ukubwa wa Tanzania.
Amesema anaunga mkono juhudi za Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo za kuongeza bajeti ya TBC ili kuimarisha uwezo wake wa kufikisha huduma ya utangazaji katika maeneo mengi zaidi ndani na nje ya nchi.
“TBC mna wajibu wa kutoa habari sahihi kwa wakati na kuhimiza uwajibikaji kwa Watanzania. Pia mnapaswa kuandaa vipindi vinavyojenga uzalendo na kuwahamasisha wananchi kuipenda nchi yao,” amesema.
Amesema chombo hicho kina nafasi muhimu katika kuelimisha umma kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025–2050, hasa wakati nchi ikijiandaa kuanza utekelezaji wa dira mpya itakayoanza Julai mwaka huu.
Pia amewahimiza watendaji wa TBC kuwa wabunifu zaidi katika kuandaa vipindi vinavyolenga vijana, ambao kwa sasa wanatumia kwa kiasi kikubwa mitandao ya kijamii kupata taarifa.
Amesema ushiriki wa vijana katika uandaaji wa vipindi unaweza kusaidia elimu kwa umma kuwafikia kwa urahisi na kwa lugha wanayoielewa.
Akizungumza kwenye mkutano huo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda amesema Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili si tu kama chombo cha mawasiliano bali pia kama rasilimali yenye thamani ya kiuchumi.
Amesema Serikali inapanga kuitangaza lugha hiyo kupitia vyombo vya habari mbalimbali ikiwemo TBC, huku kukiwa na mpango wa kufungua ofisi 10 za utangazaji katika nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Misri na Afrika Kusini.
Makonda amesema ukuaji wa shirika hilo unahitaji kuimarishwa kwa rasilimali zaidi, hivyo wizara yake inapanga kuwasilisha ombi la kuongeza bajeti ya TBC katika mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuliwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Gwakisa Mlawa amesema mkutano huo umeleta pamoja zaidi ya wadau 200 kutoka serikalini, mashirika ya umma na sekta mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha mawasiliano ya kimkakati katika utoaji wa elimu kwa umma.
