Mbeya. Yametimia. Hii ni baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kubariki adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa ndugu wawili wa kuzaliwa, waliotiwa hatiani kwa kosa la kumbaka kwa zamu mwanamke mwenye umri wa miaka 48.
Kwa hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufani, ndugu hao wawili, Furaha Mwasumbe na Nwaka Mwasumbe, wamefikia mwisho wa kupigania kuwa hawana hatia, kwani kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mahakama hiyo ndiyo ya juu zaidi.
Awali, baada ya Mahakama ya Wilaya ya Rungwe kuwahukumu kifungo cha maisha jela na kumlipa fidia ya Sh2 milioni mwanamke waliyembaka, walikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, lakini Desemba 13, 2022 walikwaa kisiki kortini.
Katika hukumu yao waliyoitoa Machi 24, 2026 na kuwekwa katika tovuti ya mahakama Machi 25, 2026, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani— Rehema Mkuye, Sam Rumanyika na Ebena Agatho, walibariki hukumu hiyo.
Simulizi la mwanamke aliyebakwa
Kulingana na ushahidi wa upande wa mashtaka, Februari 4, 2022, katika Kijiji cha Nkunga, Wilaya ya Rungwe, warufani, mmoja baada ya mwingine, walimwingilia bila ridhaa yake mwanamke mwenye umri wa miaka 48.
Siku hiyo, saa 3:00 usiku, akirudi nyumbani baada ya shughuli za soko, mwathirika wa tukio hilo, ambaye alikuwa shahidi wa kwanza, alieleza kuwa alikutana na mwendesha pikipiki anayefahamika kwa jina moja la Furaha.
Mwanamke huyo alimuomba Furaha apande pikipiki yake ili waende pamoja kwa kuwa alikuwa anaelekea mwelekeo huo, lakini wakiwa njiani, ghafla mrufani wa pili, Nwaka, alipanda pikipiki hiyo bila ridhaa yake.
Kwa mujibu wa ushahidi huo, mwanamke huyo alimuuliza Furaha kuwa mtu aliyempandisha ni nani, akamjibu kuwa anaitwa Nwaka. Hata hivyo, kwa vile alikuwa anafahamu tabia mbaya ya mrufani wa pili, hakupendezwa na hilo.
Hata hivyo, Furaha alimtoa wasiwasi kwa kumwambia kuwa kila kitu kitakuwa sawa.
Shahidi huyo alieleza kuwa siku hiyo barabara ilikuwa na matope, hivyo kuna wakati wote watatu walishuka kwenye pikipiki na kuanza kutembea kwa miguu, huku mrufani wa kwanza akikokota pikipiki.
Walipofika karibu na daraja, mrufani wa pili aliwazuia kwa mbele na kuwaambia wanapaswa kupita njia ya mkato, lakini mwanamke huyo hakukubaliana na hilo.
Hata hivyo, waliendelea kutembea na walipita karibu na duka la muuzaji anayeitwa Happy, ambapo warufani walinunua sigara. Wakiwa hapo walikutana na shahidi wa pili wa Jamhuri, Juhudi Saimon, anayefahamiana na mwanamke huyo.
Waliendelea kutembea hadi walipofika eneo linaloitwa Josho, wakati huo ikiwa imeshafika saa 10:00 usiku. Mrufani wa pili alimkaba shingo na kumuita mrufani wa kwanza akisema, “Tayari nimeshamtaiti, njoo tumbebe.”
Wote wawili walimkamata na kumpeleka kwenye mgodi wa mchanga, wakamlaza chini. Mrufani wa pili alimshikilia kwa nguvu huku mrufani wa kwanza akimvua nguo na kuanza kumbaka. Baada ya kumaliza, mrufani wa pili naye akambaka vivyo hivyo.
Alisema hakuweza kupiga kelele kwa sababu walimshika shingo kwa nguvu, na kitendo hicho kilimwacha na mikwaruzo mingi pamoja na alama shingoni.
Kulingana na kumbukumbu za kesi hiyo, siku iliyofuata, Februari 5, 2022, mwanamke huyo alitoa taarifa kwa shahidi wa nne, Hebron Mwanyumba, ambaye aliwaita wanakijiji, wakiwamo warufani, lakini walikana kutenda kosa.
Siku iliyofuata, mwathirika aliripoti tukio katika kituo cha polisi, alipatiwa fomu ya PF3, akaenda hospitali na baadaye kurudi nyumbani.
Hata hivyo, alieleza kuwa alipofika nyumbani alimkuta mrufani wa kwanza, Furaha, akizungumza na dada yake, akimwomba msamaha kwa kitendo cha kumbaka, lakini msamaha huo ulikataliwa.
Ushahidi wa mashahidi wengine
Shahidi wa pili wa Jamhuri alithibitisha kuwa Februari 4, 2022, saa 3:00 usiku, akiwa katika duka la Happy, alimuona mwanamke huyo akiwa ameongozana na warufani waliokwenda kununua sigara.
Shahidi namba tatu, ambaye ni baba mzazi wa mwanamke huyo, alieleza namna alivyoitwa na shahidi namba nne na kuelezwa kuwa mtoto wake alikuwa amebakwa na warufani, ambao walikanusha tuhuma hizo.
Shahidi namba tano, ambaye ni mchungaji, alieleza kuwa mrufani wa kwanza alimfuata Machi 15, 2022, kati ya saa 1:00 na 2:00 asubuhi, akimuomba amsaidie kwenda kwa wazazi wa mwathirika ili kuomba msamaha.
Mchungaji huyo alikwenda na kuonana na wazazi wa mwanamke huyo na kuwaeleza ombi hilo, lakini wazazi hao walimtaka asubiri kwanza hadi watakapojadili suala hilo kama familia.
Shahidi wa sita, ambaye ni mtabibu, alieleza kuwa alimchunguza mwanamke huyo Februari 5, 2022, na kubaini uwepo wa majimaji meupe ukeni pamoja na michubuko.
Katika utetezi wao, warufani walidai kuwa kuna mgogoro wa ardhi kati yao na mchumba wa mwanamke huyo, ambaye ni kaka yao kwa mama mwingine.
Baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote, iliwatia hatiani kwa kosa la ubakaji wa kundi na kuwahukumu kifungo cha maisha jela pamoja na kulipa fidia ya Sh2 milioni.
Hawakuridhika na hukumu hiyo, hivyo walikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, ambapo Desemba 13, 2022, Jaji Victoria Nongwa aliitupa rufaa hiyo, ndipo walipokwenda Mahakama ya Rufani, ambayo nayo imeitupa rufaa yao.
Miongoni mwa hoja zao za rufaa ni kwamba Jaji alikosea kisheria kwa kutupa rufaa bila kuzingatia sheria ya ushahidi, na kwamba shahidi wa kwanza alikuwa muongo.
Pia walidai kuwa ushahidi wa mashahidi ulikuwa unajikanganya kuhusu tukio la kuomba msamaha, kwani hilo halikuthibitishwa.
Walichokisema majaji wa Rufaa
Majaji walieleza kuwa watajikita katika hoja nne kuu, uaminifu wa mashahidi, utambuzi wa warufani, uwepo wa mashahidi muhimu, na uthibitisho wa kosa bila shaka.
Baada ya kuchambua ushahidi wote, waliridhika kuwa kosa lilithibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Walieleza kuwa ushahidi wa shahidi namba 1 na 3 ulikuwa thabiti, na warufani hawakuweza kuutikisa.
Kutokana na uchambuzi huo, mahakama iliridhika kuwa mashtaka yalithibitishwa ipasavyo, hivyo rufaa haina mashiko na imetupwa, huku adhabu ikibaki kama ilivyotolewa awali.
