WAZIRI wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga, ametoa wito kwa sekta binafsi kudhamini ligi za soka kutoka madaraja ya chini.
Amesema, klabu nyingi za madaraja ya chini zinakabiliwa na changamoto za kifedha ambazo zinazorotesha maendeleo yao, hali inayosababisha vipaji vya vijana wengi kushindwa kuendelezwa.
“Ushiriki wa wadau mbalimbali katika sekta ya michezo ni muhimu katika kuimarisha soka na kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji hivyo natoa wito kwenu kudhamini klabu hizo,” amesema.
Amesema, ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa michezo utachochea ukuaji wa soka na kurejesha hadhi yake ya zamani visiwani hapa.
Alisisitiza kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wadau na wawekezaji ili waweze kushiriki katika maendeleo ya michezo ikiwemo kusaidia klabu kwa vifaa, miundombinu pamoja na maandalizi ya mashindano mbalimbali.
Aidha, amesema hatua hiyo itasaidia kuibua vipaji vipya vya vijana na kuongeza ushindani katika ligi mbalimbali, jambo ambalo litachangia kuinua kiwango cha soka nchini.
Waziri Soraga amewataka viongozi wa klabu kutumia fursa ya uwepo wa wadau wa sekta binafsi kwa kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa klabu zao ili kuvutia wadhamini na wawekezaji katika maendeleo ya mchezo huo.
