. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, James Mataragio, Akimzungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa maghala na vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam Machi 25, 2026.
****
Serikali imeonya vikali wafanyabiashara wanaoficha mafuta kwa lengo la kuyauza kwa bei ya juu, ikisisitiza kuwa hakuna upungufu wa nishati hiyo nchini licha ya hali ya sintofahamu inayochangiwa na vita ya Mashariki ya Kati.
Onyo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, James Mataragio, wakati wa ziara ya ukaguzi wa maghala na vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam Machi 25, 2026.
Amesema Serikali imebaini kuwepo kwa taarifa za ucheleweshaji wa upakiaji mafuta na lawama kuelekezwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania, hali inayozua hofu isiyo ya lazima miongoni mwa wananchi.
“Hatutavumilia mfanyabiashara yeyote atakayeficha mafuta ili kujinufaisha na hali ya soko. Tutachukua hatua kali dhidi yao kama wahujumu uchumi,” amesema Dk Mataragio.
Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kujiridhisha kuhusu akiba iliyopo na kuhakikisha usambazaji wa mafuta unafanyika bila vikwazo, huku akisisitiza kuwa hakuna sababu ya wananchi kupaniki na kununua mafuta kwa wingi.
Kwa mujibu wa Serikali, akiba ya mafuta iliyopo inatosha hadi Julai 2026, huku mikakati zaidi ikiendelea kuwekwa kukabiliana na athari za vita ya Mashariki ya Kati inayoathiri soko la dunia.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, James Andilile akimzungumza.
