Dar es Salaam. Kama umefunga kamera za usalama (CCTV) nyumbani kwako, taasisi au kwenye kampuni, yapo mambo matatu ya kuzingatia ili kutoingilia faragha za watu na kuangukia kwenye mkono wa sheria.
Kwa mujibu wa Tume ya Ulinzi na Taarifa Binafsi (PDPC) mtu aliyefunga kamera za usalama nyumbani kwake, hususan getini ambapo watu hupita, anapaswa kuweka taarifa kuonyesha uwepo wa kamera katika eneo hilo.
Pia, unapofunga kamera hizo hakikisha huingilii faragha za nyumba jirani nawe, hivyo kamera imulike eneo lako pekee.
Kwa wenye taasisi za umma, kampuni au watu binafsi wanaochakata, kukusanya au kuhifadhi taarifa binafsi Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, inawalazimisha kujisajili PDPC.
Kwa mujibu wa vifungu vya 14 na 21 vya sheria hiyo, taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya, kuchakata, au kuhifadhi taarifa binafsi zinatakiwa kujisajili PDPC kupitia Mfumo wa Usajili na Uzingatiaji wa taarifa binafsi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Machi 24, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk Emmanuel Mkilia ametaja utaratibu kwa watu waliofunga kamera za usalama nyumbani ni lazima waweke taarifa ya uwepo wa vifaa hivyo eneo husika ili watu wachukue tahadhari.
Dk Mkilia ametolea mfano kamera za usalama zinazowekwa getini nyumbani kwamba kwa kuwa watu hupita eneo hilo ni lazima kuwe na taarifa ya kuwaonyeshe kuwa eneo hilo lina vifaa hivyo.
Kutoweka taarifa hizo, amesema mmiliki wa eneo husika anakuwa anaingilia faragha za watu wengine na ni kosa kisheria.
“Wapo watu wanakwenda maeneo mbalimbali kwa siri lakini baadaye taarifa zao huonekana bila ridhaa ya wahusika. Umefunga CCTV kamera yako hata kama tumepakana mimi na wewe, kamera yako inatakiwa imulike kwako si kwa mwenzio.
Kamera hizo zinapomulika kwa mwenzio unaingilia faragha yake, kwa hiyo ni muhimu kuonyesha kuwa umefunga kamera hizo,” amesema.
Akizungumzia suala la kujisajili, Dk Mkilia amesema wahusika ni taasisi zote za umma na za binafsi zinazokusanya, kuchakata, au kuhifadhi taarifa binafsi.
Kwa mujibu wa PDPC, taasisi ambazo zitabainika zinakusanya taarifa binafsi, mfano benki na hazijasajiliwa zitakabiliwa na adhabu za kisheria, ikiwemo faini kubwa na hatua nyingine za utekelezaji kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kinapiga marufuku kukusanya, kurekodi, au kusambaza taarifa za mtu bila ruhusa yake na kinaeleza adhabu yake ni faini hadi Sh50 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela, au vyote kwa pamoja.
Akifafanua zaidi, Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Tume ya Ulinzi na Taarifa Binafsi, Innocent Mungy amesisitiza wanaofunga kamera hizo kuweka ishara kuonyesha uwepo wa kamera eneo husika.
“Sheria ya wanyama inataka kama unafuga mbwa na ni mkali uweke taarifa kuwa nyumba hii inalindwa na mbwa mkali, au umeweka uzio wa umeme ni lazima uweke vibao vile kuonyesha kuwa eneo hilo ni hatari hii ndio maana yetu,” amefafanua.
Kwa wenye kuhitaji usaidizi, amesema Tume hiyo hutoa ushauri ni wapi kunapaswa kufungwa kamera za CCTV.
Amesema vifaa vya usalama haviwezi kufungwa maeneo ya siri kama vile chooni kwani ni uvunjaji wa haki ya faragha na ni kinyume na sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
“Tatizo ni ukusanyaji wa taarifa za watu kwa mfumo wa video na sauti na hapo lazima usajiliwe na uwe na hilo angalizo katika maeneo yenye kamera hizo,” amesema na kusisitiza taasisi husika zinapaswa kujisajili na Tume kabla au ifikapo Aprili 8, 2026.
Matumizi ya kamera za CCTV yanapaswa kuzingatia haki ya kikatiba ya faragha na usalama wa mtu binafsi iliyoainishwa katika Ibara ya 16 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayosisitiza haki ya kila mtu kuheshimiwa faragha yake.
Mchumi aliyejikita kwenye uchumi wa kidijitali, Francis Nyonzo amesema kitendo cha kutoa taarifa kwa wenye kamera ni utaratibu ambao unatumika karibuni dunia nzima, kwamba eneo hili lina ulinzi wa kamera.
Nyonzo amesema shida inakuja kwenye suala zima la usajili, akihoji unawezaje kumlinda mtu anayepita.
Amesema kamera hizo za CCTV zimeundwa kwa mfumo wa kulinda faragha na ndio maana picha zake si za ubora wa uangavu, bali zinakuwa ni hafifu.
“Kuhusu kutochukua picha kwa jirani tungeanzia kwenye sera za nyumba na makazi kwa sababu majengo yetu yako jirani. Jirani yako atapenda picha ichukuliwe au hatapenda, hayo ni masuala ya kujiuliza.
“Mfano nyumba moja ikiwa na umeme nyingine haina, yenye umeme ikimulika ambayo haina, basi hufurahia. Kamera kitopiga picha kwa jirani tuweke namna kuwe na makubaliano kati ya majirani.
Amesema pia ni muhimu kuwe na utaratibu, unakaa na picha za watu kwa muda gani kisha utazifuta, kwenye ufungaji wa kamera ikibidi jirani ahusishwe aone inachukua eneo lake kiasi gani.
Ameongeza ikiwezekana hata uwekwe utaratibu wa aina gani ya kamera na zitumike namna gani, hivi ndiyo vitu vya kuzingatia maana watu wanaonunua wao wananunua wanazokutana sokoni.
“Tunapaswa kujadiliana mfano kuna baadhi ya nchi wanataka kamera zinazotumika ziwe zinatoa mlio ili anayepigwa ajue amepigwa picha, wengine wakikupiga picha wanakuonesha kuwa tumekupiga picha hii, ili utoe maamuzi kama ifutwe au itumike,” amesema.
Noel Henjewele, mkuu wa kitengo cha AI na Cloud kutoka Dynatech Solutions Limited, amesema utekelezaji huu ni wa lazima na wa kimkakati kwa kuwa unaitoa Tanzania kwenye mfumo wa holela na kuingia kwenye mfumo wa kidijitali unaowajibika.
Changamoto kubwa itakuwa ni elimu kwa jamii, kwani wengi huona CCTV kama chombo cha usalama tu na si hatari kwa faragha ya jirani.
“Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa katika udhibiti kwa kuwa inazuia kurekodi watu bila sababu ya msingi (mfano, kamera inayomulika chumbani kwa jirani), italeta uwazi kwani mabango ya taarifa yanampa mtu hiyari kujua unarekodiwa.
“Vilevile kutakuwa na uwajibikaji kwa kuwa kampuni sasa zitaogopa kuvujisha namba au picha za wateja kwa hofu ya kufungiwa au kupigwa faini na Tume. Ni hatua inayozidisha nidhamu ya matumizi ya teknolojia na kulinda utu wa mtu mmoja mmoja dhidi ya ufuatiliaji usio na kikomo,” amesema Henjewele.
Ritha Rafael yeye amezungumzia upande wa uhalifu, akisema kutoa taarifa kuwa mahali Fulani kuna, kunaweza kuwafundisha wahalifu kuja na njia mbadala au kuvunja kamera pindi ili kupoteza ushahidi.
“Mimi naona hakuna haja ya kutoa taarifa popote kama kuna kamera kwa kuwa huo ni usalama mbadala, ukiachana na ulinzi wa watu au mbwa,” amesema.
Kwa upande wake Said Rashid anasema suala la kutoa taarifa ni sahihi kwa kuwa kamera hizo si za mtego, bali ni kwa ajili ya usalama.
“Kuna maeneo mengine unakuta taarifa kabisa kuwa unaingia eneo ambalo linalindwa na kamera, hivyo watu wanakuwa wanatambua. Mfano ukisema kamera imulike eneo lako tu, naona italeta wakati mgumu wakati wa kupata baadhi ya matukio ya kiushahidi na uchunguzi kwenye matukio kama ya wizi au moto,” amesema.
Amesema kamera za sikuhizi zina uwezo wa kujizungusha, hivyo kusema imulike eneo lako tu sidhani kama itatekelezeka kama ilivyopangwa.
“Wangesema kamera ziwekwe zinazohisi tukio au mtu, mfano kuna tukio inakuwa rahisi kuliko kukaa tu kufatilia eneo isilo na shughuli yeyote,” amesema.
