Dar es Salaam. Wakati juhudi za kulinda rasilimali na mazingira zikiendelea kushika kasi duniani, Afrika imetakiwa kuachana na utegemezi wa mifumo ya nje na badala yake kubuni mbinu zinazozingatia uhalisia wake wa kijamii, kiuchumi na kimazingira.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Machi 26, 2026 na wadau mbalimbali wa mazingira waliohudhuria mdahalo wa kimataifa wa siku mbili unaojadili masuala ya uhifadhi wa rasilimali na mazingira, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akizungumza katika mdahalo huo, Mhadhiri wa Idara ya Jiografia kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, Profesa Maano Ramutsindela amesema Afrika imekuwa ikiiga mifumo ya uhifadhi kutoka nje bila kuzingatia muktadha wake, hali inayochangia kushindwa kwa baadhi ya mikakati ya uhifadhi.
Amesema ni muhimu kwa bara hilo kufafanua changamoto zake za kimazingira kwa kuzingatia uhalisia wake badala ya kutegemea mitazamo ya nje ambayo wakati mwingine haiendani na mazingira ya Afrika.
“Ni lazima tuunde mifumo yetu ya uhifadhi inayozingatia rasilimali tulizonazo kama misitu, maji na wanyamapori, ili kupata matokeo chanya,” amesema Profesa Ramutsindela.
Ameongeza matumizi ya teknolojia za kisasa, tafiti za kisayansi na uchambuzi wa takwimu vinaweza kusaidia kubaini changamoto halisi na kutoa suluhisho sahihi za uhifadhi wa mazingira.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kurejesha na kuthamini maarifa ya asili ya Waafrika, akieleza kuwa mchanganyiko wa maarifa hayo na sayansi ya kisasa unaweza kuimarisha mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Pia amewataka Waafrika kuacha mtazamo wa kujiona waathirika pekee wa mabadiliko ya tabianchi na badala yake kuwa sehemu ya suluhisho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira cha Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Dk Emmanuel Sulle, amesisitiza umuhimu wa kuipa kipaumbele sauti ya Waafrika, hususan Watanzania, katika mijadala na utekelezaji wa masuala ya uhifadhi.
Amesema mfumo wa elimu unapaswa kumjenga mwanafunzi kuelewa mazingira ya Afrika kwa uhalisia wake kuanzia ngazi ya chini hadi elimu ya juu.
“Ni muhimu kujiuliza kama elimu tunayotoa inamuandaa Mtanzania kuelewa mazingira yake. Lazima iakisi hali halisi ya hapa nyumbani pamoja na maarifa ya jadi,” amesema Dk Sulle.
Aidha, amesisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha juhudi za uhifadhi, akibainisha kuwa wataalamu pekee hawawezi kuleta mabadiliko bila ushirikiano wa jamii.
“Wananchi ndio wengi na wana nafasi kubwa ya kushiriki katika kulinda rasilimali zao pamoja na kuwawajibisha viongozi,” amesema.
Ameongeza kuwa mijadala ya uhifadhi inapaswa kupanuliwa ili kuwahusisha wananchi wa kawaida, badala ya kubaki mikononi mwa wataalamu wachache.
Naye Mkuu wa Ndaki ya Sayansi ya Jamii wa UDSM, Profesa Christine Noe, ametoa wito kwa wataalamu na watunga sera kushirikiana katika kuandaa mifumo bora ya usimamizi wa rasilimali, itakayochochea maendeleo endelevu barani Afrika.
