ALAF Yaahidi Kuendelea Kuwekeza Katika Afya za Wafanyakazi Kupitia Kili Marathon

Moshi, Tanzania – Kampuni ya ALAF Limited imeahidi kuendelea kuwekeza zaidi katika afya za wafanyakazi wake kwa kuhimiza ushiriki wao katika shughuli za michezo, ikiwemo mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon zilizofanyika hivi karibuni mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza mara baada ya mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kutembelea banda la kampuni hiyo katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Meneja Rasilimali Watu wa ALAF, Jumbe Onjero, alisema kuwa ushiriki wa wafanyakazi katika matukio ya michezo husaidia kuimarisha afya ya mwili na akili, hali inayoongeza ufanisi kazini.

Alieleza kuwa pamoja na kushiriki, kampuni hiyo pia ilidhamini mbio hizo kama sehemu ya kutangaza shughuli zake, huku ikiwa na mpango wa kufungua showroom kubwa jijini Moshi ili kuwahudumia wateja wa mkoa huo na maeneo ya jirani.

Kwa mujibu wa Onjero, ALAF ilidhamini zaidi ya washiriki 50 katika mbio za mwaka huu, ambapo wafanyakazi wake walishiriki katika vipengele mbalimbali vikiwemo kilomita 42.2 (Full Marathon), kilomita 21.1 (Half Marathon) pamoja na mbio za kujifurahisha za kilomita 5.

“Tutaendelea kuunga mkono mbio hizi kwa lengo la kukuza sekta ya michezo na kuhakikisha wafanyakazi wetu wanakuwa na afya bora kupitia mazoezi,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa mwaka jana kampuni hiyo ilianzisha klabu ya jogging inayowajumuisha wafanyakazi kutoka vitengo mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kushiriki mashindano ya ndani na kimataifa, ikiwemo Kilimanjaro Marathon.

Aliongeza kuwa mwaka huu kampuni hiyo inaadhimisha miaka 65 tangu kuanzishwa kwake, jambo lililochochea kuongeza nguvu katika udhamini wa mbio hizo.

ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini katika uzalishaji wa vifaa vya chuma vya kuezekea paa, pamoja na koili za chuma zenye rangi na mabomba kwa matumizi mbalimbali ya sekta ya ujenzi. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1960, kampuni hiyo imeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.