Backer achomoa wanne Simba | Mwanaspoti

TAKRIBANI miezi mitatu imebaki kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa 2025-2026 ambapo utakwenda kushuhudia usajili wa dirisha kubwa ukifunguliwa ikiwa ni maandalizi ya mchakamchaka wa 2026-2027.

Wakati kikibaki kipindi kifupi huku duru la kwanza la Ligi Kuu Bara likimalizika kwa timu nyingi ukiiacha Simba pekee yenye mchezo mmoja pungufu, kocha mkuu wa kikosi hicho, Steve Barker inaelezwa amefanya uamuzi mapema wa kusuka jeshi lake upya huku nyota wanne wakichomolewa.

Katika uamuzi huo, tayari mchakato wa kuongezwa mikataba wachezaji likiendelea kwa wale wanaomaliza muda wao mwisho wa msimu huu na bado wanahitajika na Msauzi huyo.

Hadi sasa, Rushine De Reuck, Yusuph Kagoma na Elie Mpanzu, wameongezewa mikataba ya kuendelea kuitumikia Simba na zoezi hilo limefanyika hivi karibuni ikibaki miezi mitatu kabla ya msimu kumalizika.

Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kutoka Simba kwamba, klabu hiyo inaendelea na mchakato wa kuboresha kikosi hicho ambapo katika vikao vyao wanaangalia kila nafasi na mchango wa kila mchezaji kujua watakaoendelea nao na wapya wa kwenda kuongeza nguvu.

katika uchambuzi huo wa kina, eneo la mabeki wa kati limeonekana kuwa salama na kama hatatokea mchezaji mwingine kuumia basi asilimia ni kubwa halitapanguliwa.

Kati ya mabeki watano, watatu ni wazawa ambao ni Abdulazak Hamza na Wilson Nangu wanaouguza majeraha ambapo chanzo kutoka Simba kilisema wanaendelea vizuri, hivyo msimu ujao wanaamini watarejea kazini.

Mwingine ni beki chipukizi Vedastus Masinde aliyejiunga na klabu hiyo mwanzoni mwa msimu huu akitokea TMA Stars ya Ligi ya Championship. Masinde aliyezaliwa Juni 16, 2006 akiwa na umri wa miaka 19, anatazamwa kwa malengo makubwa ya baadaye.

Kwa upande wa mabeki wa kigeni, Rushine De Reuck raia wa Afrika Kusini, hivi karibuni amemuongezewa mkataba wa mwaka mmoja utakaoishia mwaka 2027. Mwingine ni Muivory Coast, Ismaël Olivier Touré aliyetua mwanzoni mwa msimu huu na sasa ndiye anacheza pacha na Rushine.

“Eneo hilo tumeliona lina ushindani wa hali ya juu, Nangu na Hamza wanazidi kuimarika afya zao, hivyo watarejea kazini kujiunga na wenzao msimu ujao wa 2026-2027, kutokana na hilo hatujaona sababu ya kulipangua eneo hilo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Pia wageni ambao wanacheza beki ya kati wameonyesha kiwango cha juu na ndiyo maana Rushine ameongezewa mkataba, siyo huyo pekee kila mchezaji ambaye tunahitaji kuendelea naye anaongezewa mkataba. Ukiacha huyo yupo Yusuph Kagoma na Elie Mpanzu nao wameshaongezewa mikataba.”

Chanzo hicho kimeendelea kubainisha kwamba, kiungo wa kati aliyejiunga na Simba Agosti 14, 2025, Naby Camara raia wa Guinea, kwake kuna mtihani kwani licha ya mwanzo kuonekana ni mchezaji muhimu kutokana na kucheza nafasi nyingi ikiwamo beki wa kushoto na kati mbali na ile ya kiungo ambayo ni asili yake, lakini ghafla amepoteza namba kikosini. Kupoteza namba kwa kiungo huyo kumekuja baada ya kufanyika usajili wa dirisha dogo akiletwa Nickson Kibabage upande wa beki wa kushoto akisaidiana na Antony Mligo, huku eneo la kiungo pia kukiwa na maingizo mapya.

“Camara anaonekana kutokuwa na kasi ambayo kocha anaitaka lakini pia eneo la kiungo mkabaji Barker anahitaji mtu asiye na mambo mengi na mwenye uwezo wa kucheza kwa kiwango kikubwa muda wote wa mechi bila kuchoka.

“Kwa ilivyoonekana Camara hana nafasi na ndiyo maana kocha akapendekeza asajiliwe kiungo mwingine ndipo tukafanya mazungumzo na Kelvin Nashon,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Kocha hivi sasa anahitaji kiungo mkabaji mwenye sifa hiyo kuu na sio apande juu kuchezesha timu kwani eneo la kuchezesha linajitosheleza baada ya maingizo mapya kipindi cha dirisha dogo.”

Chanzo hicho kimeeleza kwamba, kutokana na hilo, ndiyo maana hana Alassane Kante naye mwisho wa msimu huu amewekwa katika listi ya wanaoondolewa. Wengine ni Jonathan Sowah na Neo Maema anayemaliza muda wake wa mkopo akitokea Mamelodi Sundowns.

“Mpaka sasa ambao wana asilimia kubwa kuondoka ni Maema na Sowah na tayari watu wa skauti wanafanya kazi yao ya kusaka wachezaji wengine wa kuchukua nafasi zao, hao wengine lolote linaweza kutokea mbele ya safari kwani huenda kipindi hiki cha kumalizia msimu wakabadilika na kumvutia kocha,” kilisema chanzo hicho.

Simba katika usajili wa dirisha dogo Januari 2026 eneo la kiungo mshambuliaji iliwasajili Clatous Chama, Ino Loemba, Anicet Oura na Libasse Gueye ambao wote wanacheza kikosi cha kwanza na kufanya vizuri.