Bukoba. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitachukua hatua kali kwa watumishi na viongozi wa Serikali wanaoshindwa kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia fedha za Serikali, na kusababisha uwepo wa miradi ya ovyo.
Hatua hizo zitachukuliwa kwa viongozi na watumishi hao wa umma bila kujali cheo au jina la kiongozi husika, lengo likiwa ni kuhakikisha uwajibikaji ili miradi itekelezwe kwa viwango stahiki na kuleta tija.
Kauli hiyo imetolewa mjini Bukoba leo Machi 26, 2026, na Katibu Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi, baada ya kufika mkoani Kagera kuanza ziara ya siku tatu mkoani humo.
Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, Kihongosi amesema atakagua uhai wa CCM, miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali, pamoja na kufanya mikutano ya hadhara yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Kihongosi amesema chama hicho kina wajibu wa kuhakikisha yale yote yaliyoahidiwa wakati wa kampeni yanatimizwa kwa viwango, hivyo hakitakuwa tayari kuona ahadi hizo zinashindwa kutekelezwa kutokana na watumishi na viongozi wachache watakaoshindwa kutimiza wajibu wao.
Katibu Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Kenan Kihongosi akizungumza wakati alipokagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa soko la Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
“Tunakwenda kukagua miradi inayotekelezwa na fedha za Serikali, na pale tutakapokuta miradi mizuri tutapongeza, lakini penye miradi ya ovyo tutachukua hatua, kwa sababu ni wajibu wetu sisi CCM kusimamia haki na kupeleka tabasamu kwa wananchi kwa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora,” amesema.
Amesema watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa chama hicho ni kikubwa kuliko Serikali, hivyo wanapaswa kuzingatia weledi, uwajibikaji sambamba na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi.
Kihongosi amesema chama hicho ndicho chenye Serikali, hivyo suala la kukagua na kusimamia utendaji kazi wa Serikali ni la lazima kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Amesema maendeleo ya kweli ya nchi ya Tanzania yataletwa na CCM kwa kuzingatia uzoefu wake na namna chama hicho kilivyojipambanua katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uongozi wa chama kuanzia ngazi ya taifa hadi kwenye shina.
Kihongosi amewataka Watanzania kuwa na imani na chama hicho, kwani kina dhamira njema kwa nchi, huku akisema kazi ya ujenzi wa nchi inafanyika hatua kwa hatua na kwamba kina uzoefu wa kutosha katika kuendesha nchi.
“Serikali haiwezi kumaliza changamoto zote kwa wakati mmoja, kila kitu kinafanyika kwa awamu. Mfano, awamu hii tunaamua kujenga kituo cha afya, awamu ijayo tunajenga stendi, awamu hii tunajenga barabara, awamu ijayo tunajenga stendi. Ujenzi wa nchi ni kama ujenzi wa familia,” amesema.
Akikagua mradi wa ujenzi wa soko la Manispaa ya Bukoba pamoja na stendi ya mabasi, Kihongosi ameridhishwa na namna miradi hiyo inavyotekelezwa, huku akitoa agizo kwa mkuu wa mkoa pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba kuhakikisha ugawaji wa vibanda vya biashara katika soko hilo unafanywa bila upendeleo.
Ameagiza wafanyabiashara waliokuwepo sokoni hapo kupewa kipaumbele kabla ya watu wengine, ili kuondoa manung’uniko yanayoweza kutokea endapo wafanyabiashara hao hawatapewa nafasi.
“Sio kwamba wanakuja viongozi wanapewa vibanda kumi kumi na kuwaacha wale waliokuwepo hapo awali, ugawaji ufanyike bila upendeleo,” amesema.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, msimamizi wa mradi, Nixon Kissa, amesema utekelezaji wake umefika asilimia 19.45 na kwamba ulianza kutekelezwa Oktoba 2025, unatarajiwa kukamilika Januari 2027.
“Mradi unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh18.9 bilioni na utekelezaji wake unaendelea vizuri, japokuwa kuna changamoto kadhaa, ikiwemo hali ya mvua za mara kwa mara,” amesema.
Awali, Katibu wa CCM Shina namba 15 katika Kata ya Bukoba mjini Bukoba, Sajida Habibu, amesema eneo lao linakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa choo katika soko lao, changamoto iliyodumu kwa zaidi ya miaka 10, hivyo kuomba kupatiwa ufumbuzi.
