Dodoma. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametaja kitu anachokumbuka kwa mara ya mwisho alipowasiliana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi (marehemu), walikuwa na mvutano kuhusu kikao ambacho kingefanyika jana Machi 25, 2026.
Lukuvi alifariki dunia jana Jumatano Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa alikokuwa akipatiwa matibabu kwa kinachoelezwa kuwa alipatwa na tatizo la shambulio la moyo.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi, nyumbani kwa marehemu Area D jijini Dodoma, Machi 26, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Dk Mwigulu ametaja mvutano huo leo Machi 26,2026 akisema ulikuwa wa heri kwani yeye alitaka kuahirisha kikao cha jana lakini akasema kuwa Lukuvi alijenga hoja ya kutaka kikao kisiahirishwe na hivyo wakakubaliana kiwepo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu hakutaja kikao hicho kilihusu nini na wapi wangekutana ingawa Lukuvi alikuwa ni waziri anayefanya kazi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akimfariji, Germina Lukuvi (wa tatu kushoto), mjane wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi alipokwenda nyumbani kwa marehemu Area D jijini Dodoma kuhani, Machi 26, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
“Tulipanga kuwa na kikao siku ya jana, mimi nilikuwa napambana kukiahirisha na yeye alipambana kikao kiwepo, kwa hiyo katika mvutano huo, alijenga hoja ikabidi nami nikubali,” amesema Dk Mwigulu.
Amewataka viongozi wa Serikali na vyama kuendelea kufika nyumbani kwa marehemu Lukuvi na kuwafariji wafiwa akisema katika kipindi hiki, Serikali itakuwa bega kwa bega na familia ili kuhakikisha kila jambo linakwenda vizuri.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akimfariji, Germina Lukuvi, mjane wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi alipokwenda nyumbani kwa marehemu Area D jijini Dodoma kuhani, Machi 26, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Wengine waliofika asubuhi ya leo ni Spika wa Bunge, Mussa Zungu ambaye hakuzungumza chochote, zaidi ya kuwapa pole mke na familia ya Lukuvi kisha akaondoka.

