Halmashauri Ya Geita Yatangaza Nafasi za Kazi 15, Mwisho wa Maombi Aprili 5, 2026

Halmashauri ya Manispaa ya Geita imetangaza nafasi 15 za kazi kwa Watanzania wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi mbalimbali zilizotangazwa rasmi na Mkurugenzi wa Manispaa.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa Machi 23, 2026, nafasi hizo zinajumuisha kada za Dereva Daraja II (nafasi 5), Dereva Mitambo (Plant Operator) nafasi 3, Mwandishi Mwendesha Ofisi Daraja la II (Secretary) nafasi 2, pamoja na Msaidizi wa Kumbukumbu Daraja la II (Records Management Assistant) nafasi 5.

Kwa nafasi ya Dereva Daraja II, waombaji wanatakiwa kuwa na cheti cha kidato cha nne pamoja na leseni ya daraja E au C, uzoefu wa kuendesha gari usiopungua mwaka mmoja bila kusababisha ajali, pamoja na mafunzo ya msingi ya udereva kutoka vyuo vinavyotambuliwa na Serikali kama VETA au vingine.

Kwa upande wa Dereva Mitambo, waombaji wanatakiwa kuwa na kidato cha nne, leseni ya daraja G ya uendeshaji mitambo na uzoefu wa angalau miaka mitatu bila ajali. Aidha, wanapaswa kuwa na ujuzi wa kutunza na kuendesha mitambo.

Kwa nafasi ya Mwandishi Mwendesha Ofisi Daraja la II, waombaji wanapaswa kuwa na kidato cha nne au sita pamoja na stashahada (NTA Level 6) ya Uhazili. Vilevile wanapaswa kuwa na ujuzi wa kompyuta pamoja na uwezo wa kuandika kwa kasi ya maneno 80 kwa dakika katika Kiswahili na Kiingereza.

Kwa nafasi ya Msaidizi wa Kumbukumbu Daraja la II, waombaji wanatakiwa kuwa na kidato cha nne au sita pamoja na stashahada katika Utunzaji wa Kumbukumbu, pamoja na ujuzi wa kompyuta.

Tangazo hilo pia limeweka masharti ya jumla kwa waombaji, likiwataka wawe raia wa Tanzania, wasizidi umri wa miaka 45, na kuwasilisha nyaraka sahihi ikiwa ni pamoja na vyeti vya taaluma vilivyothibitishwa. Aidha, hati za matokeo zisizo rasmi kama vile “statement of results” hazitakubaliwa.

Waombaji wametakiwa kuwasilisha maombi yao kupitia mfumo wa kielektroniki wa ajira (Recruitment Portal) kupitia https://portal.ajira.go.tz/
kabla ya mwisho wa kutuma maombi uliowekwa kuwa Aprili 5, 2026.

Halmashauri hiyo imeonya kuwa maombi yatakayowasilishwa nje ya utaratibu ulioainishwa hayatazingatiwa, huku ikihimiza waombaji kuhakikisha wanakamilisha maombi yao kwa usahihi na kwa wakati.