Mara nyingi mijadala ya maendeleo ya uchumi huzungumzia miradi mikubwa inayoweza kuonekana kwa macho kama barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege au miradi ya nishati, pengi ni kwakuwa inahusisha uwekezaji mkubwa na kugusa sekta nyingi za uchumi.
Mbali na miradi hiyo mikubwa, kuna nguvu nyingine ya miundombinu ambayo haijengwi kwa saruji wala chuma na haihitaji mitambo mikubwa ya ujenzi, bali ipo katika simu za mkononi zinazotumiwa na mamilioni ya watu kila siku.
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za Desemba 2025 zinaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na zaidi ya akaunti milioni 76.5 za huduma za fedha kwa simu katika mitandao mbalimbali.
Mkurugenzi wa M-Pesa Tanzania, Epimack Mbeteni, anasema nguvu hiyo inatokana na maendeleo ya huduma za fedha kwa njia ya simu ambazo zimebadilisha namna watu wanavyofanya miamala na kushiriki katika shughuli za uchumi.
“Kuna nguvu zinazochochea uchumi kwa sauti kubwa kama miradi mikubwa ya miundombinu au mageuzi ya sera. Lakini pia kuna nguvu zinazofanya kazi kimya kimya, zikiwa zimejikita katika maisha ya kila siku ya wananchi na athari zake ni kubwa katika mabadiliko ya uchumi,” anasema Mbeteni.
Kwa mujibu wa Mbeteni, huduma za fedha kwa simu zimekuwa sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania kwa sababu zinawapa wananchi wengi zaidi fursa ya kushiriki katika mfumo wa kifedha bila kujali wanapoishi au kiwango cha kipato walicho nacho.
Anasema huduma za fedha kwa simu zilipoanza kutumika nchini mwaka 2008, zilionekana zaidi kama njia mbadala ya kutuma au kupokea fedha kwa haraka. Wakati huo, wananchi wengi walizitumia kama mbadala wa kubeba fedha taslimu au kutuma pesa kwa ndugu walioko mbali.
“Huduma hizi zilipoanza, zilionekana kama urahisi tu wa kutuma na kupokea pesa tu. Wachache walitarajia kwamba zingekuja kuwa sehemu muhimu ya shughuli za kila siku za uchumi,” anasema bosi huyo wa M-Pesa inayotawala soko kwa asilimia 41.2.
Aidha mbeteni anasema kama ambavyo miundombinu mingine huchochea na kurahisisha biashara kwa, kupunguza gharama na kufungua fursa za biashara za kikanda, M-Pesa nayo kwa namna yake inafanya hivyo, inaweka urahisi wa miamala yote ya kibiashara na huduma za kifedha kwa ujumla wake.
Kama ambavyo bandari zinaunganisha Tanzania na biashara ya kimataifa, huduma za kifedha kwa njia ya simu zinaunganisha wasio na akaunti za benki na biashara rasmi na wakati gridi za umeme zikiwezesha uzalishaji viwandani.
Kwa upande wa biashara, jukwaa la M-Pesa Business limewasaidia wafanyabiashara kupokea malipo kwa njia ya kidijitali na kusimamia fedha zao kwa ufanisi zaidi.
Kupitia M-Wekeza, watumiaji wanaweza kuwekeza kiasi kidogo cha fedha na kupata faida. M-Koba inasaidia vikundi vya kijamii kuweka akiba kwa pamoja, huku Songesha ikitoa mikopo midogo ya muda mfupi kwa watumiaji wanaokabiliwa na changamoto za kifedha za muda.
Aidha, mfumo wa miamala ya simu iliyounganishwa na mfumo wa malipo ya Serikali, unawawezesha wananchi kulipia huduma mbalimbali za serikali moja kwa moja kupitia simu zao.
“Huduma hizo ni zile zote ambazo taasisi za Serikali hutoa ‘control number’ ambazo ni pamoja na malipo ya pasi za kusafiria, kodi ya ardhi na faini mbalimbali za serikali,” anasema Mbeteni.
Mbeteni anasema M-Pesa pekee imechangia kuunda ajira na fursa za kipato kwa maelfu ya watu nchini. Kwa mujibu wa Mbeteni, huduma hiyo inahusisha zaidi ya mawakala 200,000 na wafanyabiashara zaidi ya 600,000 wanaotumia mfumo huo katika shughuli zao za kila siku.
“Katika nchi ambayo mara nyingi maendeleo hupimwa kwa miradi mikubwa ya miundombinu, huduma za fedha kwa simu zinawakilisha aina nyingine ya miundombinu ya kidijitali ambayo inapatikana kwa watu wengi na kusambaa kila mahali,” anasema.
Mbeteni anasema, mchango wa miamala ya simu unaweza usionekane moja kwa moja kama daraja au reli mpya, lakini athari zake zinaonekana katika uimara wa biashara ndogo, kuongezeka kwa shughuli za kifedha na kuimarika kwa ushiriki wa wananchi katika uchumi.
