Dar es Salaam. Serikali imeanza maandalizi ya kutumia dawa mpya ya sindano ya Lenacapavir kama njia mbadala ya kinga dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), hatua inayotarajiwa kurahisisha ufuasi wa tiba kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu jijini Dodoma, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema Lenacapavir italenga zaidi watu walio katika hatari kubwa ya maambukizi ya VVU pamoja na wagonjwa waliopata usugu wa dawa za kufubaza virusi (ARVs).
Ameeleza kuwa, tofauti na dawa za sasa zinazohitaji kumezwa kila siku, Lenacapavir hutolewa kwa njia ya sindano mara mbili kwa mwaka, kila baada ya miezi sita, jambo linalopunguza mzigo wa matumizi ya dawa za kila siku na hivyo kuongeza uwezekano wa watu kuzingatia matibabu au kinga.
Kwa matumizi ya kinga (PrEP), Msasi amesema mtu atapewa sindano mbili za Lenacapavir kwa mwaka, kila moja ikiwa na dozi ya miligramu 464 kila miezi sita.
Kwa sababu dawa hutolewa mwilini taratibu, ameasema mtu anapopewa sindano ya kwanza anapaswa pia kumeza vidonge vinne (miligramu 300 kila kimoja); viwili siku ya kwanza na viwili siku ya pili, ili kufikia kiwango kamili cha ulinzi ifikapo siku ya tatu.
Sindano ya pili hutolewa baada ya wiki 24 hadi 26 bila haja ya vidonge tena. Iwapo mtu atapitisha zaidi ya wiki 26, itamlazimu aanze upya, amesema.
Kisayansi, amesema Lenacapavir ni dawa ya kundi la capsid inhibitors, inayofanya kazi kwa kuzuia kirusi cha VVU kushikamana na kuingia ndani ya seli za kinga za mwili (CD4). Kwa kufanya hivyo, virusi hushindwa kujizalisha na kusambaa mwilini.
“Kirusi hakiwezi kuishi bila kuingia kwenye seli. Dawa hii inazuia hatua hiyo hakishikamani, hakiingii na hakiwezi kujizalisha,” amefafanua na kuongeza:
“Hata kama kirusi kimeingia mwilini, dawa inakizuia kisizaliane. Mwisho wa siku kinadhoofika na kuondolewa mwilini,” anasema.
Mbali na kinga, dawa hiyo pia itatumika kwa wagonjwa ambao tayari wameambukizwa VVU lakini wanapata changamoto ya usugu wa dawa nyingine. Katika hali hiyo, Lenacapavir husaidia kudhibiti uzalishaji wa virusi na kuimarisha afya ya mgonjwa.
Anasema tofauti na dawa nyingi za sasa zinazohitaji matumizi ya kila siku, Lenacapavir hutolewa kwa njia ya sindano mara mbili tu kwa mwaka, hali inayotarajiwa kuongeza ufuasi wa matibabu na kupunguza changamoto ya wagonjwa kusahau au kuchoka kutumia dawa.
“Ni mageuzi makubwa. Tunazungumzia mtu anayepata sindano moja na inamlinda au kumtibu kwa miezi sita. Hii inabadilisha kabisa mtazamo wa matibabu ya VVU,” anasema Msasi.
Anaongeza uwezo huo unaifanya dawa hiyo kutumika katika nyanja mbili kuu: kama kinga (PrEP) kwa watu walio katika hatari ya kuambukizwa na pia kama tiba kwa wagonjwa waliopata usugu wa dawa nyingine.
Dawa hiyo yenye uwezo wa kutumika kama mbadala wa ARVs kwa wenye maambukizi ya VVU, ilionyesha ufanisi mkubwa katika tafiti za awali, likiwemo jaribio lililofanyika Uganda mwaka 2025.
Licha ya ufanisi wake, Msasi amesisitiza kuwa Lenacapavir si tiba ya kuondoa VVU mwilini, bali ni sehemu ya matibabu endelevu yanayosaidia kudhibiti virusi na kuwawezesha wagonjwa kuishi maisha marefu na yenye afya.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (APHFTA), Dk Egina Makwabe licha ya kusema ujio wa dawa ya Lenacapavir ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya VVU, ipo haja ya kupunguza gharama ili iweze kuwafikia Watanzania wengi.
Amesema pamoja na ubora wake, dawa hiyo ina changamoto ya gharama kubwa inayokadiriwa kufikia kati ya Sh40 milioni hadi Sh50 milioni kwa miezi sita kwa mtumiaji mmoja, hali inayoweza kuifanya ishindwe kufikiwa na wananchi wengi.
Kutokana na hali hiyo, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama hizo ili kuwezesha watu wengi zaidi, hususan wale walio katika makundi hatarishi na taaluma zinazowaweka kwenye mazingira ya hatari ya maambukizi, kunufaika nayo.
Akijibu suala la gharama, Msasi amesema hospitali binafsi hazihusiani na Serikali na kwamba hizo zinafanya biashara.
“Mnufaika yeye ataamua akatibiwe private (hospitali binafsi) au hospitali za umma. Sisi tunapeleka hospitali zenye makubaliano na Serikali, sehemu kubwa wanaotumia ARV wanatibiwa ndani ya vituo vya Serikali, Aphtha hao wanafanya biashara, taratibu zote zinazotumika za utoaji wa ARV nchini zitatumika hivyo hivyo kama PrEP,” amesema Msasi.
Pamoja na hayo, Dk Makwabe amesema chama hicho kimewahamasisha wanachama wake kuanza mchakato wa kuagiza dawa hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu zote za kisheria zilizowekwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA).
“Tunaipongeza serikali kwa kuruhusu dawa hii kuingia nchini kwa ajili ya kusaidia wananchi. Hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha matumizi yake yanazingatia miongozo ili kuepusha matumizi yasiyo sahihi ambayo yanaweza kusababisha usugu wa dawa,” amesisitiza.
Aidha, amesema APHFTA itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanachama wake wanaofuata taratibu wanapata fursa ya kuagiza na kusambaza dawa hiyo kwa ubora unaotakiwa.
Baada ya dawa hiyo kupitishwa kimataifa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Tanzania kuhakikisha inasajiliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), hivyo kufungua milango kwa wahitaji kuipata pindi taratibu nyingine zitakapokamilika.
“Hivi sasa mtu yeyote mwenye uwezo wa kuileta nchini anaweza kufanya hivyo kwa kufuata taratibu zilizowekwa. Lakini sisi kama Serikali tunaenda mbali zaidi kuhakikisha inaingizwa rasmi kwenye mfumo wa huduma za afya,” anasisitiza Msasi.
Anaongeza mwongozo wa kitaifa wa matibabu (treatment guidelines) umehuishwa na unatarajiwa kusainiwa kabla ya Juni mwaka huu, ambapo Lenacapavir itaingizwa rasmi kama sehemu ya huduma za VVU.
Hata hivyo, Msasi anasema bado kuna mazungumzo yanaendelea ili dawa hiyo iingizwe kwenye mfumo wa ugavi wa serikali.
Amesema Tanzania bado inategemea ufadhili wa dawa za VVU kupitia Global Fund, hivyo ujumuishaji wa Lenacapavir unahitaji makubaliano katika awamu mpya ya ufadhili inayotarajiwa kujulikana kama GC8.
“Tunaamini katika mazungumzo haya tutaweza kuingiza Lenacapavir kama sehemu ya dawa za kinga ya VVU, kama ambavyo WHO inapendekeza,” anasema.
Katika hatua nyingine, Msasi amesema Serikali inakusudia kuondoa mfumo wa vituo maalumu vya CTC, ambavyo vilikuwa vinatengwa mahsusi kwa huduma za VVU, badala yake huduma zote sasa zitaunganishwa katika mfumo mmoja wa utoaji huduma hospitalini.
“Hakutakuwa tena na sehemu maalumu ya kusema hapa ni kwa wagonjwa wa VVU. Mgonjwa wa malaria, nimonia au VVU wote watahudumiwa sehemu moja na daktari yuleyule,” anasema.
Anafafanua hata utoaji wa dawa utaunganishwa, ambapo wagonjwa wote watapokea dawa zao dirisha moja, hatua inayolenga kuondoa unyanyapaa uliokuwa ukisababisha baadhi ya watu kujificha au kutoendelea na matibabu.
Kwa kupunguza unyanyapaa na Lenacapavir, Msasi amesema vitaongeza kwa kiasi kikubwa ufuasi wa matibabu na kupunguza usugu wa dawa.
“Kadri unavyopunguza marudio ya matumizi ya dawa, ndivyo unavyoongeza ufuasi. Hii itasaidia pia kupunguza usugu wa dawa kwa sababu wagonjwa hawatakosa dozi mara kwa mara,” anasema.
Ameongeza Serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza unyanyapaa, ambao bado ni kikwazo kikubwa kwa baadhi ya watu.
Akizungumzia huduma za kinga (PrEP), Msasi anasema mfumo uliopo umefanikiwa kusogeza huduma karibu na walengwa, ikiwemo katika maeneo ya kijamii kama baa na sehemu za starehe.
Anasema mfumo huo huo utatumika kusambaza Lenacapavir pindi itakapoanza kutolewa rasmi kama kinga.
“Mwenye uhitaji anajua wapi pa kupata huduma. Tumezisogeza karibu na wananchi, na hilo ndilo tutakalofanya pia kwa Lenacapavir,” amesema.
“Wakati tunaanza kutoa PrEP ilikuwa mtu wa kawaida asiende kwenye kituo kwa ajili ya kufuata dawa kwa sababu na yeye ataonekana kama ni mtu ambaye ameathirika, tukarahisisha ukifuatilia PrEP zinatolewa kwenye maeneo wahusika waliko…
“Kwa kuweka kumbukumbu sawa, hatuna changamoto za PrEP mpaka muda huu tunavyoongea, yaani tunahofia tutakuwa na changamoto ya dawa hizi kuisha muda wake lakini si kukosekana,” amesema
Kuhusu changamoto za matumizi ya kila siku ya dawa hadi baadhi ya watu kuchoka, kusahau au kukumbwa na changamoto nyingine, Msasi anasema Lenacapavir ni suluhisho kubwa.
