Global Publishers
March 26, 2026
0 Comments
Dar es Salaam – Msanii na mchekeshaji maarufu, Juma Lokole, amegusa hisia za mashabiki baada ya kuonekana akimwaga machozi ya furaha kufuatia kupewa zawadi ya gari katika sherehe ya siku yake ya kuzaliwa.
Tukio hilo la kipekee limefanyika katika hoteli ya kifahari ya Serena Hotel, ambapo Lokole alikuwa ameandaa hafla maalum ya “Birthday Dinner” iliyohudhuriwa na marafiki, watu wa karibu na wadau mbalimbali wa burudani.
Imebainika kuwa zawadi hiyo ya gari ilitolewa na kampuni moja inayojihusisha na huduma za kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya kumthamini na kumuunga mkono msanii huyo katika kazi zake za burudani.
Kwa mujibu wa video zilizosambaa mitandaoni, Lokole alionekana kushindwa kujizuia baada ya kutangaziwa zawadi hiyo kubwa, hali iliyomfanya kumwaga machozi mbele ya wageni. Tukio hilo lilizua hisia miongoni mwa waliohudhuria, wengi wakimpongeza na kumtakia heri katika maisha yake na kazi yake ya sanaa.
Sherehe hiyo iligubikwa na burudani, muziki na mshangao mbalimbali, lakini zawadi ya gari ndiyo iliyochukua uzito mkubwa wa usiku huo na kuwa gumzo mitandaoni.
Mashabiki wengi wameeleza kufurahishwa na tukio hilo, wakisema ni ishara ya kuthamini juhudi za msanii huyo ambaye amekuwa akitoa burudani kwa muda mrefu nchini.
Bila shaka, birthday hiyo imeacha kumbukumbu ya kipekee kwa Juma Lokole, huku ikiwa ni moja ya matukio yaliyovutia hisia za wengi ndani na nje ya mitandao ya kijamii.