Kocha ataja kinachombeba Diarra | Mwanaspoti

UTOFAUTI wa viwango vya magolikipa wa kigeni na wazawa, umeelezwa upo katika nidhamu ya muendelezo wa kile wanachokifanya uwanjani pamoja na bidii ya kutokuridhika na mafanikio kidogo.

Kocha wa makipa wa Mbeya City, Patrick Mwangata, amesema wazawa walio wengi wanaridhika mapema, tofauti na wageni wanaoboresha viwango vyao ambapo kila msimu wanakuja na kitu kipya hali inayofanya kujiwekea heshima ya kipekee.

β€œUkiondoa golikipa Aishi Manula ambaye alikaa nje kutoka na majeraha, wengi wao hawana muendelezo wa viwango, ukitofautisha na wageni mfano Djigui Diarra tangu ajiunge na Yanga mwaka 2021 amekuwa na ubora wa hali ya juu, ndiyo maana anaitwa katika timu ya taifa lao la Mali,” amesema Mwangata na kuongeza;

β€œMfano msimu uliopita wazawa kama Patrick Munthari wa Mashujaa ndiye alikuwa na cleansheet nyingi ambazo ni 12, alifuatiwa na Yona Amosi wa Pamba alikuwa na 11, Yakoub Suleiman wa Simba alimaliza na nane wakati ambao anaichezea JKT Tanzania.

β€œAnayefanya vizuri hadi sasa ni Amosi ambaye ana cleansheets tano, huo ni uthibitisho wa utofauti wa muendelezo wa viwango vyao, Diarra msimu uliopita alimaliza nafasi ya pili nyuma ya Moussa Camara aliyekuwa na 19, huku Diarra akiwa nazo 17 na sasa ni kinara ana 10.”

Katika hilo, Munthari alikiri kwa kusema: β€œNi kweli hatuna muendeleozo wa viwango kwa sababu tofauti, ukiondoa Simba na Yanga ambazo zina kipa namba moja wanaofahamika, binafsi najiona msimu huu siwezi kuzifikia cleansheet nilizomaliza nazo msimu uliopita, siwezi kuweka sababu zangu wazi.”