Lukuvi Kuagwa Dodoma, Dar Kuzikwa Iringa Jumanne Machi 31, 2026

Global Publishers
March 26, 2026
0 Comments

Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi (70), utazikwa katika kijiji cha familia yake, Idodi, wilaya ya Iringa Vijijini, siku ya Jumanne, Machi 31, 2026.

Lukuvi, ambaye pia alikuwa mbunge wa Isimani (CCM), alifariki dunia saa 1 asubuhi ya jana, Jumatano, Machi 25, 2026, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mshtuko wa moyo.

Leo, Alhamisi, Machi 26, 2026, imebainika ratiba ya mazishi ya Lukuvi:

  • Ijumaa, Machi 27, 2026 – Mwili wa Lukuvi utaagwa na wabunge katika Viwanja vya Bunge, Dodoma.
  • Jumamosi, Machi 28, 2026 – Mwili wake utaagwa jijini Dar es Salaam, katika Viwanja vya Karimjee.
  • Jumapili, Machi 29, 2026 – Mwili wa Lukuvi utasafirishwa kwa ndege hadi Iringa Mjini, na kesho yake, Machi 30, utapokelewa na wananchi katika eneo la Gangilonga kabla ya kupelekwa kijijini kwao, Idodi.

Lukuvi aliongoza jimbo la Isimani kwa zaidi ya miaka 31 kuanzia mwaka 1995 na alikuwa mbunge mkongwe zaidi katika Bunge la Tanzania. Mazishi yake yatahusisha viongozi mbalimbali wa serikali, ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aliacha watoto watatu na mjane mmoja, akiacha historia ya uongozi wa muda mrefu na mchango mkubwa katika siasa za Tanzania.