Kilombero. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amesema mvua kubwa iliyonyesha usiku wa Machi 24 imesababisha kukatika kwa barabara kuu ya Ifakara – Mlimba katika maeneo ya Mbingu, Chita na Njage, hali iliyosababisha magari, yakiwemo mabasi ya abiria kushindwa kupita.
Akizungumza baada ya kukagua miundombinu ya barabara hiyo iliyoharibika leo Alhamisi Machi 26, 2026, Kyobya amesema kutokana na changamoto ya usafiri iliyojitokeza, kwa sasa usafiri wa treni ya reli ya kati maarufu ‘kipisi’ utatumika kusafirisha wananchi, ikifanya safari kila siku kati ya Mlimba na Ifakara.
“Wakati wataalamu na mafundi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) wakiendelea na matengenezo ya kuunganisha barabara hii ya Ifakara – Mlimba, tumeona tutumie treni hii ili iweze kusafirisha wananchi. Itafanya safari kila siku hadi barabara itakapokuwa imerekebishwa, hivyo nawaomba wananchi wawe wavumilivu katika kipindi hiki,” amesema Kyobya.
Muonekano wa Barabara ya Ifakara – Mlimba eneo la Mbingu iliyokatika badala ya mvua kubwa kunyesha usiku wa Machi 24 na kusababisha wananchi kutumia usafiri wa treni maarufu ‘kipisi’ kwenye reli ya Tazara. Picha Hamida Shariff
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wataalamu wa Wakala wa Taifa wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuongeza kasi ya ukarabati ili kuhakikisha barabara hiyo ambayo ni kiungo muhimu cha uchumi kwa Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla, inarejea katika hali yake ya kawaida haraka iwezekanavyo.
Kyobya amesema tangu mvua hiyo kubwa iliyonyesha Machi 24, haijanyesha nyingine ingawa baadhi ya maeneo yanaendelea kujaa maji kwa sababu yapo mabondeni.
Akizungumzia kaya 100 zilizoathirika na mafuriko, amesema baada ya hali ya hewa kutengemaa kwa siku mbili mfululizo, waathirika wengi wameanza kurejea kutoka makazi ya muda waliyokuwa wamehifadhiwa na kurudi kwenye makazi yao ya kudumu.
“Kwa kiasi kikubwa wengi wamerejea kwenye makazi yao na wanaendelea kusafisha nyumba zao ili kuendelea na maisha ya kawaida. Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usalama imejipanga kuhakikisha wananchi wa Ifakara na wilaya nzima wanakuwa salama wakati wote,” amesema.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua, hususan kuepuka kuvuka maji na kuwa makini na watoto wadogo.
Pia ametoa tahadhari kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao katika mito mikubwa wilayani humo, akibainisha kuwa kipindi cha mvua ni hatari kutokana na kujaa kwa maji yenye mkondo mkali.
Kwa upande wa afya, Kyobya amewahimiza wananchi kuzingatia kanuni za usafi ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko, ikiwemo kipindupindu na kuhara, huku akiwaagiza maafisa afya kuendelea kutoa elimu ya usafi wa mazingira, matumizi sahihi ya vyoo na ulazima wa kuchemsha maji ya kunywa.
Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya (wa kwanza kulia) akiangalia mtambo unaotengeneza barabara ya Ifakara – Mlimba eneo la Mbingu iliyokatika kutokana na mvua zinazoendelea kwenye wilayani humo. Picha Hamida Shariff
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Folkward Mchami amesema tangu kutokea kwa mafuriko hayo, wamekuwa wakihakikisha misaada mbalimbali inawafikia waathirika, ikiwemo kuwapatia malazi ya muda, chakula, magodoro na mahitaji mengine ya msingi.
Amesema halmashauri imetenga maeneo maalumu kwa kaya zote zilizopoteza makazi au zilizoathiriwa na maji, huku akitoa wito kwa wadau na wasamaria wema kujitokeza kusaidia.
“Nawaomba wasamaria wema kujitokeza kuchangia misaada kwa waathirika wa mafuriko, ikiwemo mavazi, chakula na vifaa vya shule, kwani wapo watoto waliopoteza madaftari, vitabu, sare na vifaa vingine vilivyosombwa na maji,” amesema Mchami.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Dk Erick Atugonza amewataka wananchi kutumia dawa za kutibu maji zinazopatikana katika ofisi za kata, pamoja na kuzingatia usafi binafsi.
“Ni muhimu kunawa mikono kwa maji tiririka kabla na baada ya kula, kuchemsha maji ya kunywa na kutumia vyandarua hasa katika kipindi hiki ambacho mazalia ya mbu yanaongezeka, ili kujikinga na malaria,” amesema Dk Atugonza.
Kwa upande wake, mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo, Mwanahawa Ally mkazi wa Kijiji cha Machipi, ameishukuru Serikali na wasamaria wema kwa msaada wanaoendelea kutoa tangu walipopata mafuriko Machi 24 mwaka huu.
Amesema pamoja na nyumba kujaa maji na nyingine kubomoka, wakazi wengi wamepata hasara kubwa ya mazao hasa mpunga na mahindi, baada ya mashamba mengi yaliyopo mabondeni kufurika na mazao kusombwa na maji.
