Mawio na machweo ya William Lukuvi: Pumzika Mwana-Ismani

Dar es Salaam. Mwandamizi mkuu amekiacha chumba. Kiti kimoja ukumbini sasa ni tupu. Kitahitaji kujazwa. William Vangimembe Lukuvi, mbunge mwenye uzoefu mkubwa zaidi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amevuta pumzi ya mwisho. Kifo ni hatima ya uhakika kwa binadamu wote, kila mja hugota kwa namna na wakati wake.

Mahali roho ya Lukuvi iliacha mwili ni Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma. Sababu ya kifo ni shambulio la moyo. Machi 25, 2026, saa 1 asubuhi, ndiyo tarakimu za Lukuvi duniani, zilifikia hitimisho. Aliishi duniani miaka 70, miezi 7 na siku 10. Huo ndiyo mzingo wa maisha ya Lukuvi.

Tangu Bunge la 12, lililoanza kazi Novemba 2020, Lukuvi alikuwa ndiye mbunge mwandamizi zaidi, Bunge la Tanzania. Kutokana na sifa hizo, Lukuvi aliweza kuongoza Bunge katika uchaguzi wa kuwapata maspika watatu; Job Ndugai na Dk Tulia Ackson (Bunge la 12), vilevile Mussa Zungu (Bunge la 13).

Lukuvi alikuwa mbunge kwa miaka 30 iliyotimia. Tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1995, katika uchaguzi mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi vya siasa Tanzania, hakuwahi kupoteza kiti. Lukuvi na wananchi wa Jimbo la Isimani, Iringa, wametenganishwa na kifo.

Lukuvi alianza kuwa mwanachama wa Tanganyika African National Union (Tanu). Kadi ya Tanu aliichukua mwaka 1973. Mwaka 1977, baada ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichopatikana kwa muunganiko wa vyama vya Tanu na Afro Shiraz Party (ASP), Lukuvi, alijisajili uanachama CCM. Alibaki mwana-CCM mpaka kifo kilipomchukua.

Mwaka 2001, Lukuvi alishinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM (NEC). Alibaki mjumbe wa NEC hadi mauti yake. Mwaka 2010, Lukuvi aliingia kwa mara ya kwanza Kamati Kuu CCM (CC), aliendelea kuwa mjumbe wa mkutano huo nyeti kwenye chama, mpaka alipovuta pumzi ya mwisho.

Ndani ya Bunge, Lukuvi alipata kutoa huduma kwenye kamati za kudumu tofauti. Mwaka 2005 mpaka 2010, Lukuvi alikuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Mwaka 2015 hadi 2018, alikuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Lukuvi ameacha mjane, Germina Lukuvi na watoto. Jambo moja ambalo huwezi kumnyima Lukuvi sifa yake ni namna alivyoweza kumudu kubaki kwenye baraza la mawaziri, vipindi vya misukosuko ya kisiasa, mwaka 2010 – 2015. Alikuwa mwanasiasa aliyeweza kuchomoza majira yote.

Aliweza kuaminiwa na marais watano tofauti; Ali Hassan Mwinyi aliyemteua kuwa mkuu wa wilaya, Mkapa unaibu waziri na uwaziri, Kikwete ukuu wa mkoa na uwaziri, Magufuli uwaziri na Rais Samia katika nafasi ya uwaziri, mshauri wake wa siasa, kisha tena uwaziri mpaka alipofumba macho kwa mara ya mwisho.

Upande wa siasa za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, tangu alipofariki dunia veterani wa siasa, Joseph Mungai mwaka 2016, Lukuvi alionekana kuwa mmoja wa wanasiasa viranja kwenye kanda hiyo, hasa Mkoa wa Iringa. Hata hivyo, ni dhahiri wino wa historia ya binadamu, lazima utakoma mahali pumzi inapokata.

Kijiji cha Mpogoro, kata ya Idodi, wilaya ya Iringa Vijijini, ndiyo kila kitu kuhusu Lukuvi kilianza. Mawio yakawa Agosti 15, 1955. Imempendeza Mungu machweo ya Lukuvi yawe Machi 25, 2026. “Nayo mavumbi kurudi ardhini kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa,” imeandikwa katika Mhubiri 12:7.

Safari ya elimu ya Lukuvi ilianzia Shule ya Msingi Kitanewa, Iringa, kuanzia mwaka 1962 na kuhitimu mwaka 1970. Mwaka 1974, alijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) na kuhitimu astashahada mwaka 1975. Mwaka 1982 mpaka 1983, alisoma Shule ya Juu ya Momsomol, Moscow, Urusi, alikohitimu stashahada ya juu ya sanaa, sayansi ya siasa.

Mwaka 1999 hadi 2001, Lukuvi alisoma na kuhitimu shahada ya kwanza ya masomo ya kimataifa na diplomasia, Chuo Kikuu cha kimataifa cha Washington, kilichopo British Virgin Islands. Mwaka 2008 mpaka 2011, Lukuvi alidahiliwa na kuhitimu shahada ya uzamili ya sanaa, sayansi ya siasa.

Kati ya mwaka 1975 na 1980, Lukuvi alikuwa mwajiriwa wa Wizara ya Elimu, akiwa mwalimu wa elimu ya msingi. Mwaka 1980 mpaka 1984, Lukuvi alikuwa mwajiriwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwa Katibu ya Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), ngazi ya wilaya na mkoa, katika vipindi tofauti.

Kati ya mwaka 1984 hadi 1989, Lukuvi alikuwa mkuu wa idara, makao makuu CCM, Dodoma. Mwaka 1993 mpaka 1994, Lukuvi alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa. Mwaka 1994, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Kagera. Alitumikia nafasi hiyo mpaka mwaka 1995, alipogombea ubunge na kushinda.

Mwaka 1995 mpaka 2000, Lukuvi alikuwa Naibu Waziri wa Vijana, Kazi na Ajira. Mwaka 2000 hadi 2005, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sera, Uratibu, na Masuala ya Bunge. Kati ya mwaka 2006 na 2008, Lukuvi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Halafu, mwaka 2008 mpaka 2010, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kutoka mwaka 2010 mpaka 2015, Lukuvi alihudumia wizara moja tu, akiwa waziri kamili, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Masuala ya Bunge. Mwaka 2015 mpaka 2022, alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Halafu, kuanzia mwaka 2024 mpaka mauti yalipomfika, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, na Masuala ya Bunge.

Kikokotoo cha miaka kitakuonesha kuwa ndani ya miongo mitatu, tangu Uchaguzi Mkuu 1995, Lukuvi ndiye amekuwa mnadhimu mkuu wa Serikali bungeni aliyehudumia kwa muda mrefu zaidi. Jumla miaka 12. Alitumikia nafasi hiyo kipindi cha marais watatu, Benjamin Mkapa (2000 – 2005), Jakaya Kikwete (2015 – 2021), halafu Rais Samia Suluhu Hassan (2024 – 2026).

Tangu mfumo wa vyama wa vyama vingi vya siasa urejee, Lukuvi alikuwa mjumbe wa baraza la mawaziri chini ya marais wote; Mkapa (2000 – 2005), kabla ya hapo alikuwa naibu waziri. Kikwete (2010 – 2015), kabla ya hapo alikuwa mkuu wa mkoa. Magufuli (2015 – 2021), Rais Samia (2021 – 2022), halafu (2024 – 2026). Kati ya mwaka 2022 – 2024, Lukuvi alikuwa mshauri wa siasa wa Rais Samia.

Safari njema William Vangimembe Lukuvi.