Mkenya awachongea Guede, Rupia | Mwanaspoti

KOCHA wa Singida Black Stars, Mkenya David Ouma amesema safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inatakiwa kuongeza umakini wa kutumia vizuri nafasi zinazotengenezwa, huku washambuliaji, Elvis Rupia na Joseph Guede, wakikabiliwa na kibarua kizito.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, bado hajaridhishwa kwa kiasi kikubwa na eneo lote la ushambuliaji, ingawa kwa kipindi hiki cha mapumziko ya muda mfupi anaendelea kuyafanyia kazi.

“Kwa washambuliaji tulionao na idadi ya mabao tuliyofunga haiendani na nafasi zinazotengenezwa, mtu anaweza kuzungumzia kuhusu eneo pia la kujilinda, ni kweli, japo makosa tunayofanya ni machache tofauti na ya ushambuliaji,” alisema Ouma.

Ouma alisema katika kipindi hiki cha kupisha mapumziko ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hawatakuwa na muda wa kupoteza, kwani wataendelea na mazoezi kwa ajili ya kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza raundi ya kwanza.

“Tuna wiki moja mbele yetu kabla ya kucheza na Azam FC, ni mechi ngumu sana na muhimu kwetu hasa ukizingatia tunacheza nyumbani, tunataka kuanza raundi ya pili vizuri, hivyo ni lazima turekebishe changamoto zetu tulizonazo,” alisema Ouma.

Katika mechi 15 za raundi ya kwanza ilizocheza timu hiyo, imeshinda saba tu, sare nne na kupoteza pia nne, ikiwa nafasi ya sita na pointi zake 25, imefunga mabao 18, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.

Kauli ya Ouma inatokana na mwenendo usioridhisha wa washambuliaji wa kikosi hicho, ambapo Rupia aliyefunga mabao 10, ya Ligi Kuu akionyesha kiwango bora msimu uliopita wa 2024-2025, msimu huu wa 2025-2026, amefunga mawili tu.

Kwa upande wa Guede, aliyewahi kutamba na Yanga kisha kujiunga na Singida aliyoachana nayo Januari 23, 2025 na kutua Al-Wehdat SC ya Jordan kabla ya kurejea kikosini hapo Januari 2026, hadi sasa amefunga bao moja tu la Ligi Kuu.

Winga, Mossi Nduwumwe, aliyejiunga na kikosi hicho Januari 2026, akitokea Flambeau du Centre FC ya kwao Burundi, ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi, akiwa nayo matatu ya Ligi Kuu Bara, sawa na beki wa kushoto, Mghana Ibrahim Imoro.