Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limekamata pikipiki 115 na watuhumiwa tisa katika operesheni maalumu iliyovunja mtandao wa wizi na usambazaji wa pikipiki nchini.
Akizungumza jana Machi 25, 2026 katika Kituo Kikuu cha Polisi Iringa, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Allan Bukumbi, alisema operesheni hiyo ilianza Januari 17, 2026 Kihesa, ikihusisha ufuatiliaji wa kina uliobaini mtandao uliokuwa ukifanya kazi kwa siri kwa muda mrefu.
Alisema wahusika walitumia mbinu za hali ya juu, ikiwemo kughushi nyaraka za usajili ili kuficha uhalisia wa pikipiki hizo.
Katika hatua za awali, watuhumiwa watatu walikamatwa wakiwa na pikipiki tatu zilizoibwa, na mahojiano yao yalibaini kila mmoja alihusika katika wizi wa zaidi ya pikipiki 50 pamoja na utengenezaji wa kadi bandia kwa ajili ya kuuza mali hizo.
Uchunguzi zaidi uliwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wengine wawili wanaodaiwa kuwa wanunuzi wakuu, huku upekuzi ukizaa pikipiki 82, vibao vya namba, kadi bandia, mashine ya kuoshea magari na zaidi ya Sh6.4 milioni zinazodaiwa kuwa mapato ya uhalifu huo.
Pia, lilikamatwa guta lililotumika kusafirisha pikipiki hizo. Uchunguzi umebaini mtandao huo ulikuwa na matawi katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro na maeneo mengine, huku baadhi ya watu wakidaiwa kufadhili shughuli hizo.
Pikipiki 115 zilizokamatwa kwa wizi zikiwa zimehifadhiwa kituo cha Polisi mkoani Iringa. Picha na Mtandao
Kamanda Bukumbi alisema juhudi zinaendelea kuwabaini na kuwachukulia hatua wote waliohusika, akiwataka wananchi waliopoteza pikipiki kufika kituoni kwa utambuzi.
Aliongeza kuwa operesheni inaendelea, huku akisisitiza ushirikiano wa wananchi katika kukomesha uhalifu.
