Mwasa: Mbeya City ishuke daraja? Subiri muone kazi

BEKI wa kati wa Mbeya City, David Mwasa amesema licha ya presha wanayopitia ya matokeo yasiyoridhisha, suala la timu hiyo kushuka daraja ni ndoto kwani mechi zilizobaki zinaweza kubadili upepo na kurejesha furaha kikosini.

Pia staa huyo wa zamani wa Mbao FC, amesema kwa sasa wanaendelea na matizi kujifua kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya KMC kuhakikisha wanaianza safari mpya ya matumaini Ligi Kuu.

Mbeya City ambayo imerejea Ligi Kuu msimu huu, haijawa na mwenendo mzuri ikiwa nafasi ya 14 katika msimamo kwa pointi 13 baada ya kucheza mechi 16 na kuweka presha ndani na nje ya uwanja, huku baadhi wakiikatia tamaa.

Mwasa ameliambia Mwanaspoti kuwa, kinachowatokea kwa sasa ni sawa na timu nyingine Ligi Kuu kwani ligi hiyo imeonekana kuwa ngumu na si kwao tu japokuwa wanaendelea kujifua kuhakikisha wanabaki salama.

Amesema wanaoitabiria kushuka daraja wasubiri kwani michezo 14 waliyonayo inaweza kubadili upepo na kuleta furaha kwa mashabiki na kikosi kwa ujumla, akieleza kuwa wao wachezaji wanayo matumaini ya kufanya vizuri.

β€œTunaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao Aprili 3 dhidi ya KMC, tunajua ni mechi nzuri yenye ugumu kutokana na hali ya timu zote lakini sisi wachezaji tunaamini Mbeya City haiwezi kushuka daraja.

β€œUkiangalia matokeo ya timu nyingi si mazuri sana, tunazidiana pointi chache, anayeshinda mechi mbili anapanda nafasi zaidi juu, hatujapoteza malengo wala mwelekeo na tunaomba sapoti zaidi ya mashabiki,” amesema beki huyo.