Ikiwa imepita takribani mwezi mmoja tangu kuzuka kwa mvutano wa kijeshi katika ukanda wa Mashariki ya Kati unaohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran, athari zake zimeanza kuonekana katika soko la mafuta duniani na kuzusha hofu ya mfumuko wa bei.
Mpaka jana Machi 25, bei ya pipa moja ya mafuta ghafi ilifikia Dola 89 kwa pipa ikipungua kutoka Dola 97 Machi 08, hata hivyo kiwango kama hicho kilishuhudiwa zaidi ya mwaka 2022 wakati vita vya Russia na Ukraine viliposhika hatamu.
Kwa Tanzania, hatari hiyo ni halisi kutokana na utegemezi wa mafuta kutoka katika baadhi ya nchi zilizo ndani ya eneo hilo la mzozo. Hali hii imeanza kuathiri mwenendo wa soko la kimataifa, ikiongeza presha katika gharama za usafirishaji, uzalishaji na maisha ya kila siku ya wananchi.
Katika mazingira kama hayo, mjadala mkubwa unakuwa ni kwa namna gani nchi imejipanga kukabiliana na ongezeko la bei za vitu ikizingatiwa kuwa mafuta ni nishati muhimu katika uchumi.
Wachumi wanashauri hatua za haraka zichukuliwe ili kupunguza athari kwa walaji, ikiwemo kupitia upya mfumo wa kodi kwenye mafuta ili kushusha makali ya bei kwa muda.
Lakini pia inapendekezwa kuongeza kiwango cha uagizaji wa mafuta ili kujenga akiba ya kutosha, sambamba na kuongeza bajeti ya ununuzi wa nishati hiyo ili kuhakikisha upatikanaji wake hauathiriki katika kipindi hiki cha sintofahamu ya kimataifa.
Kwa mtazamo wa muda mrefu, wadau wanasisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika gesi asilia na nishati mbadala, hatua inayoweza kusaidia kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje na kuimarisha uthabiti wa uchumi wa taifa.
Mchambuzi wa uchumi na biashara, DK Lutengano Mwinuka amesema katika hatua za muda mfupi ni vyema kuangalia namna ya kucheza na mifumo ya kikodi ili itoe majibu ndani ya muda mfupi wakati hali ikiwa mbaya iwe rahisi kujua nini cha kufanyika.
“Tujue tunafanya nini kwani mafuta yana athari kubwa katika upande wa usafirishaji tujue ni kwa kiasi gani lakini tujue tuna mfumo gani wa kumeza hali hii kwa kipindi cha muda mfupi,” anasema.
Jambo hilo litasaidia kupunguza makali ya bei kwa muda mfupi kwani mafuta yana athari katika sekta ya usafirishaji na hivyo kuweka uwezekano wa kugusa bei za bidhaa nyingine.
Hilo lifanyike wakati ambao nchi inaangalia namna inavyoweza kuongeza hifadhi ya mafuta yake kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
Kwa sasa Tanzania imekuwa ikiagiza mafuta ya kutumia kwa miezi mitatu ambayo huenda kama bei ikiongezeka inakuwa ni rahisi kuathiriwa ndani ya muda mfupi.
“Kuongeza uwezo wa kufanya uhifadhi mzuri zaidi, hili lifanyike wakati ambayo nchi za Afrika ziangalie namna ambayo zinaweza kuwekeza katika kuchuja mafuta ambayo yatawezesha upatikanaji kwa njia za karibu zaidi,” anasema.
Alitolea mfano wa nchi kama Libya, Angola na Nigeria kuwa na mafuta ambayo yangeweza kutumika kwa nchi nyingine za Afrika ikiwa uwekezaji utafanyika.
“Pia kuna haja ya kujenga mahusiano mazuri na wauza bidhaa za mafuta ambao bei zao zinatabirika hii inaweza kuwa njia nzuri ya kukabiliana na hali hii, kuwa na wabia ambao wanaweza kuleta mafuta kwa haraka itakapohitajika,” anasema.
Kuhusu uhifadhi wa mafuta ya kutosha uliotajwa na Dk Lutengano tayari serikali imeanza jitihada za kuongeza matanki ambayo yatatumika kuhifadhi mafuta.
Machi 3 mwaka huu, Rais Samia amezindua mradi wa ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 378,000.
Mchambuzi wa uchumi Profesa Aurelia Kamuzora anaangalia suala hili kwa mtazamo mpana wa kihistoria na kiuchumi, akieleza kuwa utegemezi wa mafuta unatokana na mifumo ya uzalishaji iliyoachwa tangu enzi za ukoloni.
Anasema hali hiyo imefanya hata teknolojia za viwanda na utaalamu wa wahandisi vimejengwa kuzunguka matumizi ya mafuta, hali inayofanya iwe vigumu kubadilika kwa haraka.
Anasisitiza kuwa ili kujikwamua, ni lazima kuwekeza katika teknolojia mbadala na kuanza kujenga uwezo wa ndani wa uzalishaji wa nishati.
Kamuzora anaona gesi asilia kuwa fursa muhimu kwa Tanzania, akipendekeza kuimarishwa kwa miundombinu ya usambazaji wa gesi na kuifanya ipatikane kwa bei nafuu ili iwe mbadala wa mafuta katika matumizi mbalimbali, ikiwemo usafiri na viwanda.
Pia anasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika nishati mbadala kama umeme wa jua, ambayo inaweza kupunguza utegemezi wa mafuta kwa kiasi kikubwa.
“Hata kama mafuta yataendelea kuagizwa ni lazima kuwe na mbadala wa uhakika ili kupunguza madhara ya mishtuko ya bei,” anasema.
Katika kuimarisha suluhisho la ndani, Kamuzora anahimiza kuendelezwa kwa ubunifu wa teknolojia za ndani, akiwataka vijana wabunifu kuungwa mkono ili kuleta suluhisho zinazotokana na mazingira ya Tanzania.
Njia nyingine zinazoweza kupunguza athari hizo ni kuweka hatua za makusudi zinazoweza kupunguza matumizi ya mafuta ikiwemo kuimarisha usafiri wa umma ndani ya miji ili watu wasione ulazima wa kutoka na magari binafsi.
Hali hii itapunguza kiwango cha mafuta kinachotumika kwani watu wengi wanatumia usafiri mmoja tofauti na kila mtu angewasha gari yake.
Kwa upande wake, Mchambuzi wa Uchumi, Oscar Mkude anasema Tanzania haitaathirika na kupanda kwa bei ya mafuta pekee bali hata mbolea.
Hiyo ni kwa sababu mapigano haya yanavuruga minyororo ya ugavi wa bidhaa kama mafuta ya petroli, dizeli, mafuta ya taa na mafuta ya ndege, Mbolea kama kiungo muhimu katika shughuli za kilimo na baadhi bidhaa za vyakula vinavyoingizwa kutoka.
Anasema kulingana na hali iliyopo mafuta husababisha shinikizo la haraka kwenye viwango vya bei na pia ni vigumu kudhibiti kwa muda mrefu.
“Kimsingi, sera bora ingekuwa ni kubaini minyororo mbadala ya ugavi, kwa mfano kutoka kwa wazalishaji wa ndani ya Afrika. Hata hivyo, chaguo hizi ni chache na wakati mwingine ni ghali zaidi,” anasema.
Hivyo, kinachobaki ni hatua za muda mfupi kama kuweka akiba ya kutosha ya mafuta kwa miezi kadhaa Lakini akiba hiyo ikiisha nchi itakuwa kwenye hatari zaidi.
“Kwa hiyo, hatuwezi kuepuka umuhimu wa kuwa na minyororo mbadala ya ugavi kama suluhisho la kuaminika la kupata mafuta. Mwisho wa siku, kilicho muhimu ni upatikanaji wa bidhaa, si bei yake. Serikali inaweza na inapaswa kuzingatia kuhakikisha upatikanaji zaidi kuliko bei,” anasema.
Anasema watu wanaweza kuzoea na kukabiliana na mabadiliko ya bei ingawa ni kwa maumivu lakini ni vigumu zaidi kukabiliana na ukosefu wa bidhaa kabisa.
Hali hii pia inahusu mbolea na bidhaa za chakula hivyo kwa muda mrefu nchi itakumbwa na mfumuko wa bei kutokana na vita vinavyoendelea.
“Hili hatuwezi kuliepuka kadri vita vitakavyoendelea. Tunachopaswa kuepuka ni hali ya kukosa kabisa mafuta nchini.,” anasema.
Anasema kwa muda mrefu zaidi ni vyema kuboresha na kuharakisha miradi ya gesi asilia (LNG), ambayo inaweza kusaidia matumizi ya ndani na pia kuiwezesha nchi kunufaika na hali kama hizi.
Historia inaonyesha kwamba hali kama hizi hujirudia kila baada ya miaka michache na Wanaofanikiwa ni wale wanaojifunza mapema na kujiandaa ipasavyo, pamoja na kuchukua fursa za baadaye.
Kuhusu mbolea anasema, Tanzania ilikuwa na fursa ya kuanzisha mradi wa gesi kwenda mbolea kati ya mwaka 2015 hadi 2022.
“Bado kuna matumaini ya kutekeleza mradi huu wa kimkakati. Hata hivyo, muda ni mdogo kabla miradi kama hii kupoteza mvuto kwa wawekezaji, kwani teknolojia ya hidrojeni ya kijani (green hydrogen) inaonekana kuwa chaguo bora zaidi kutokana na kuwa rafiki kwa mazingira,” anasema.
Kwa upande wa vyakula, kwa kiasi kikubwa anasema nchi inaweza kubadilisha na kutumia bidhaa mbadala zinazopatikana ndani ya nchi.
“Funzo kuu katika mfumo mpya wa dunia ni kwamba ili kuwa imara, tunahitaji kulinda na kuhakikisha usalama wa minyororo yetu ya ugavi, ikiwa ni pamoja na kuibadilisha na kuipanua. Si salama tena kutegemea chaguo moja tu. Mambo hubadilika haraka na kama huna mbadala, wewe ndiye unayeathirika zaidi,” anasema.
Katika kukabiliana na suala hili, Mkude anasema ruzuku sio suluhisho kwa aina ya tatizo hili. “Unatoa ruzuku kama unajua, kwa mfano, ni njaa ya mpito wakati watu wanasubiri mazao yakauke. Yaani baada ya kipindi kinacho weza kukisiwa tatizo litakuwa limeisha”
“Ukiweka ruzuku kwenye mafuta na bei ikaendelea kupanda, wakati unasitisha ruzuku bei inaweza kuwa mara dufu zaidi. Hii italeta ugumu katika mtazamo ya kisiasa serikali iliyo madarakani inaweza kupata ugumu wa kushughulika na mitazamo hasi kutoka kwa wananchi,” anasema.
Anasema moja ya njia ya kushughulika na suala hili ni kuacha watu wajifunze kukabiliana na mabadiliko ya bei na endapo Serikali ikiamua kuingilia ni lazima iwe na uhakika kuwa hali itakuwa shwari na si mbaya.
