OFISI YA MBUNGE CHATO KUSINI YAFURAHISHWA KUKABIDHIWA MAJENGO YA TANROADS

…………..

OFISI ya Mbunge wa Jimbo jipya la Chato Kusini imeshuhudia utiaji saini wa makabidhiano ya majengo ya Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Geita dhidi ya Halmashauri ya wilaya ya Chato.

Makabidhiano hayo yamefanyika kutokana na kukubaliwa kwa maombi ya halmashauri ya wilaya hiyo kutaka kutwaa majengo yaliyojengwa katika mradi wa Barabara kuu ya Bwanga hadi Biharamulo kwa kiwango cha lami.

Mradi huo ulihusisha barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo kilometa 112 ambapo ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga ikiwa na urefu wa kilometa 45 na barabara ya Bwanga-Biharamulo ikiwa na urefu wa kilometa 67 chini ya mkandarasi wa kampuni ya Synohydro Corporation.

Katika utekelezaji wa mradi huo, pia ulihusisha ujenzi wa nyumba mbalimbali za watumishi zilizojengwa kwenye Kata ya Buziku ikiwa ni kambi kuu katika mradi huo na eneo la kuhifadhia mitambo mbalimbali ya ujenzi.

Kutokana na kukamilika kwa maradi huo mwaka 2017, halmashauri ya wilaya ya Chato ikalazimika kuomba kukabidhiwa majengo hayo kwaajili ya kuendeleza miradi mingine ya kijamii kwa manufaa ya wananchi na serikali kwa ujumla.

Akisaini makubaliano ya kukabidhiwa rasmi majengo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato, Geraid Mgoba, ameishukuru serikali kuu kwa kukubali kuyakabidhi majengo hayo kwa halmashauri ili yaweze kusaidia katika miradi ya kijamii.

Hata hivyo, wawakilishi kutoka hazina chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya fedha walikuwa ni Ismael Ogaga na Mohamed Said huku Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini ikiwakilishwa na Katibu wa Mbunge Joseph James.

Wengine ni Ofisa tawala wa wilaya ya Chato, Alexander Msisiri, pamoja na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Photunatus Jangole.