INAELEZWA kwamba, mshambuliaji wa Coastal Union, Adam Salamba, ameamua kujiweka kando na timu hiyo kwa sasa, baada ya kudaiwa hajamaliziwa kiasi cha fedha za usajili walizokubaliana awali, tangu amejiunga na kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’, Agosti 1, 2025.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa kikosi hicho, umeliambia Mwanaspoti kwamba, Salamba ameondoka kambini na hayupo na nyota wenzake wanaojiandaa na mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba itakayochezwa Aprili 2, 2026, hadi atakapokamilishiwa fedha zake.
“Ni kweli kuna fedha za usajili anazotudai, ambazo hata hivyo nisingependa kuziweka wazi, mchakato wa kumlipa unaendelea na tutaukamilisha kwa haraka iwezekanavyo, nadhani angeendelea na mazoezi kuliko kujiweka kando,” kilisema chanzo hicho.
Kiongozi mmoja aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, aliliambia Mwanaspoti kilichosababisha mchezaji huyo kugoma na kujiweka kando na timu hiyo, ni kutokana na baadhi ya wachezaji wenzake kulipwa stahiki zote, tofauti na yeye aliyepewa ahadi tu.
“Malipo ya wachezaji wa msimu huu yalikuwa yanalipwa tofauti kwa sababu kuna wengine walikuwa wanalipwa moja kwa moja na uongozi wa timu, ila wengine walipewa stahiki zao na watu binafsi, sasa hii iliibua shida kidogo,” alisema kigogo huyo.
Salamba alijiunga na kikosi hicho, Agosti 1, 2025, baada ya kutokuwa na timu tangu mara ya mwisho alipoachana na Al-Brans SC ya Libya, huku akiwahi kuzichezea pia, Stand United FC, Lipuli FC, Namungo FC na Simba zote kutoka Tanzania.
Timu nyingine alizowahi kuzichezea mshambuliaji huyo ni Al-Jahra SC ya Kuwait, JS Saoura ya Algeria, Ghazl El Mahalla ya Misri na Libyan Stadium aliyoachana nayo na kutimkia Al-Brans ya Libya pia kisha kuondoka na kutua Coastal Union msimu huu.