Simulizi ya manusura maafa Rungwe, vifo vikiongezeka

Mbeya. Simanzi, vilio na majonzi vimetanda katika Kata za Lupepo na Nkunga wilayani Rungwe mkoani Mbeya, kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyosababisha vifo vya watu 20 na kuacha majeruhi watano, baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha usiku wa kuamkia Machi 25, 2026.

Awali, taarifa zilieleza kuwa watu 18 walipoteza maisha katika tukio hilo, lakini idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 20, kulingana na maelezo ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jafari Haniu, aliyethibitisha leo Alhamisi Machi 26, 2026.

Amesema vifo hivyo vyote vinatoka katika kata za Lupepo, Nkunga, Kawetele na Ikuti, ambazo zimeathirika zaidi na janga hilo la asili, lililosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo hayo ya Nyanda za Juu Kusini.

Mwandishi wa Mwananchi aliyetembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika ameshuhudia hali ya huzuni ikitawala, huku shughuli za misiba zikiendelea katika kaya zilizopoteza ndugu na jamaa, na wengine wakiendelea na maziko ya wapendwa wao waliopoteza maisha kwa ghafla.

Hali ilikuwa mbaya zaidi katika Kata za Lupepo na Nkunga, ambako vilio, taharuki na majonzi vilitawala kila kona, wananchi wakionekana kukata tamaa huku wakikabiliana na athari za tukio hilo.

Wananchi waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti katika vijiji hivyo, wameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kuiomba Serikali kuingilia kati haraka ili kuwasaidia waathirika, hasa katika kuboresha miundombinu iliyokwamisha juhudi za uokoaji.

Wamesema changamoto ya barabara mbovu na miundombinu duni imekuwa kikwazo kikubwa kwa timu za uokoaji kufika kwa wakati katika maeneo yaliyoathirika, hali iliyochangia ugumu wa kuwafikia waathirika na kuokoa maisha zaidi.

Aidha, wameitaka Serikali kuchukua hatua za muda mfupi na muda mrefu ili kuhakikisha usalama wa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya kina ya maeneo yenye uwezekano wa kukumbwa na majanga kama hayo na kuweka mikakati ya kuyazuia au kupunguza athari zake.

Emanuel Martin, mkazi wa Nkunga anasema Machi 25 itabaki katika historia yake baada ya kuwapoteza watu wanne wa familia yake katika maporomoko hayo, tukio alilodai ni la kwanza kutokea kijijini hapo.

Amesema katika maafa hayo amewapoteza baba yake mdogo, mke wa baba yake mdogo, mtoto wao na mjukuu.

“Bora kama wangeumwa hata kidogo, hii inaumiza sana, wote hawa walikuwa wazima kabisa, naiomba Serikali itutazame sisi wanafamilia tuliobaki, hatuna kitu tumebaki wakiwa,” amesema Martin huku akibubujikwa machozi.

Amesema mvua hiyo ilianza kunyesha saa 4 usiku, lakini haikuwa kubwa kabla ya hali kubadilika saa 8 hadi 9 usiku udogo ulipoanza kuporomoka na kuangukia nyumba yao ambayo marehemu wote walikuwa ndani.

“Tunaumia sana kuipoteza familia yetu, baba, mama, dada na mjukuu, nyumba nayo imeanguka na hakuna mali yoyote tuliyotoa, Serikali itusaidie kuona tunatokaje katika kipindi hiki kigumu,” amesema Martin.

Mkazi mwingine wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Martin Solomon (78), amesema amepoteza wajukuu wake watatu waliokuwa wamelala naye katika nyumba moja,  baada ya kuangukiwa na kifusi kwenye chumba walikokuwa wamelala.

Amesema watoto hao wamefariki dunia baada ya maporomoko ya udongo kuangukia nyumba yao na kuwasababishia umauti.

Solomoni amesema wakati mvua ikiendelea kunyesha, maji yalijaa kwa kasi kwenye vyumba vya nyumba yake, hali iliyomuwia ugumu kutoa msaada kwa watoto hao, licha ya kufanya jitihada za kuokoa maisha yao.

“Kwa sasa kuna mmomonyoko mkubwa sana wa udongo huko mlimani, hali hii inasababisha maporomoko kwa sababu kuna mvua kali. Jana maji yalijaa sana tukashindwa kupenya popote hadi wajukuu zangu wakafa kwa maji,” amesema Martin huku akiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara kurahisisha huduma za uokoaji wakati wa majanga kama hayo.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, mkazi mwingine wa eneo hilo, Eston Mwangama amesema baada ya mvua kuongezeka usiku, wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi, waliamka na kuanza kupita nyumba kwa nyumba kutoa msaada kwa waliokumbwa na madhara.

Amesema ongezeko la vifo limetokana na kukatika kwa mawasiliano kati ya vitongoji na vijiji, kufuatia madaraja na barabara kuharibika kutokana na mvua hiyo.

“Kwa maana hiyo, wale tuliokuwa tunawaokoa tulishindwa kuwafikisha katika Kituo cha Afya Lupepo. Barabara zote na madaraja mengi yanayotuunganisha yamekatika, msaada ulikuwa mdogo na kwingine haukuwepo kabisa,” amesema Mwangama.

Ameongeza kuwa tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa wananchi kuanza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu yao bila kusubiri wafadhili na pia Serikali kuangalia namna ya kusaidia kutokana na jiografia ya eneo hilo lenye milima mikubwa na mikali.

Kwa upande wake, Jesca David amesema changamoto kubwa ni miundombinu duni ya barabara, akieleza kuwa mazingira ya maeneo mengi si rafiki na hivyo kuhatarisha maisha ya wakazi wa maeneo hayo.

Ameiomba Serikali kuvipa kipaumbele vijiji hivyo ili kunusuru maisha ya wananchi wengi, akibainisha kuwa licha ya kuchangia pato la Taifa kupitia shughuli za kilimo, bado wanakabiliwa na tatizo la miundombinu ya barabara sambamba na huduma za kijamii.

“Huduma za kijamii ni ndogo sana huku. Tunafanya shughuli za kilimo kwa sehemu kubwa sana, sasa tunatamani Rais (Samia Suluhu Hassan) apange siku moja aje aone mazingira yetu na haya yaliyotokea,” amesema Jesca.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amesema:

“Tumepokea taarifa ya vifo vya watu wengine wawili baada ya kuangukiwa na udongo usiku na watu hao wametambuliwa kwa majina ya Rachel George (9), mwanafunzi wa Mhule ya Msingi Songwe na Isac George wote wa familia moja,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Mbali na taarifa hiyo, Haniu ametoa rai kwa wananchi kuhama maeneo hatarishi katika kipindi hiki mvua zinapoendelea kunyesha, ili kuepuka madhara zaidi yanayoweza kutokea.

Haniu amesema wakati wananchi hao wakiondoka maeneo hatarishi, Serikali inaendelea kuangalia cha kufanya ili kunusuru maisha ya wakazi hao kwa siku zijazo.

“Naomba wananchi tuchukue tahadhari, hatutaki kuona madhara au athari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, mvua ni nyingi kwa sasa,” amesema Haniu.

Mapema, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lupepo, Lusajo Mwafyela amesema wamepata  pigo kubwa kwa jamii na uongozi wake kwa kuwa katika eneo lake watu sita wamefariki dunia kutokana na tukio hilo.

Amesema kila familia imefanya mazishi kwa utaratibu wake, akibainisha kuwa maporomoko hayo yamesababisha takribani nyumba 13 kubomoka na nyingine kuharibika vibaya.

“Tunaiomba Serikali iwasaidie waathirika waliopoteza mali, nyumba na ndugu zao, ili kuona namna ya kuwafariji. Kwangu ni pigo kubwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa, kwani hali kama hii haijawahi kutokea kwa miaka yote ya mababu,” amesema Mwafyela.