Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema inaendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika visiwani humo, huku ikiahidi kuwa ifikapo mwaka 2028 tatizo hilo litakuwa historia.
Hatua hiyo imekuja wakati Zanzibar ikiendelea kutegemea umeme unaosafirishwa kutoka Tanzania Bara kupitia nyaya za chini ya bahari, hali inayokabiliwa na changamoto kutokana na miundombinu iliyochoka na kufikia ukomo wa matumizi.
Kwa mujibu wa Serikali, kwa sasa Unguja inapokea umeme kupitia nyaya mbili za baharini; moja yenye uwezo wa megawati 45 iliyowekwa mwaka 1980 na ambayo tayari imetumika kwa asilimia 98.8, na nyingine yenye uwezo wa megawati 100 iliyofikia matumizi ya asilimia 97.3. Nyaya hizo zimeelezwa kufikia ukomo wa uwezo wake wa kusafirisha umeme.
Akizungumza leo Alhamisi Machi 26, 2026 wakati wa ziara maalumu ya kukagua miradi ya umeme katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), Haji Haji amesema Serikali imeanza kutekeleza miradi mbalimbali ya kuzalisha na kusambaza umeme kwa lengo la kuondoa changamoto hiyo.
Amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa ufadhili wa washirika wa maendeleo pamoja na fedha za ndani, ikiwa ni jitihada za kuziba pengo lililopo katika upatikanaji wa umeme.
“Serikali imesaini mkataba na kampuni ya Marekani wenye thamani ya dola milioni 64 (sawa na Sh164 bilioni) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme kisiwani Pemba,” amesema.
Kituo cha kusambazia umeme kilichopo Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja. Picha na Zuleikha Fatawi
Kwa upande wa Unguja, amesema Serikali imetiliana saini mkataba na kampuni ya India wenye thamani ya dola milioni 159 (Sh408 bilioni) kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umeme wa jua katika eneo la Matemwe, kitakachozalisha megawati 30 ifikapo Septemba mwaka huu.
Haji alieleza kuwa pamoja na uzalishaji, Serikali pia inatekeleza mradi wa uhuishaji wa njia kuu za usafirishaji wa umeme, hasa katika maeneo ya Kaskazini na Kusini Unguja ambako miundombinu iliyopo imefikia ukomo.
Amesema kwa sasa kila upande una njia mbili za megawati 17 ambazo haziwezi tena kupitisha mahitaji mapya ya umeme, hivyo kuna ulazima wa kuboresha miundombinu hiyo ili kuongeza uwezo wa usafirishaji.
Ameongeza kuwa baadhi ya miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo haikugusa maeneo yote yenye uhitaji, jambo lililolazimisha Serikali kutumia fedha zake kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka megawati 17 hadi 30.
Katika hatua nyingine, Haji amesema kituo cha umeme cha Bambi kinatarajiwa kuzalisha megawati 40, ambapo 20 zinatarajiwa kuanza kupatikana ifikapo Julai mwaka huu.
Alifafanua kuwa tayari ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bambi hadi Uroa umeanza, ambapo umeme huo utaunganishwa kwenye gridi ya taifa.
Aidha, amesema kituo cha Matemwe kitaunganishwa na njia ya Mangapwani na kuingia kwenye gridi, huku akieleza kuwa kuna uwezekano wa kupatikana hadi megawati 50 kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Kwa upande wa nishati jadidifu, amesema mradi wa umeme wa upepo katika eneo la Makunduchi unatarajiwa kuzalisha megawati 120 ndani ya kipindi cha miezi minane na kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa.
Haji amebainisha kuwa Serikali pia inapanga kuweka mifumo ya betri za kuhifadhi umeme katika maeneo ya Bambi na Makunduchi ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaendelea hata wakati wa changamoto za jua au upepo.
Akizungumzia miradi hiyo, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif amesema utekelezaji wake utaondoa kwa kiasi kikubwa changamoto ya umeme visiwani humo.
Ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuendelea kushirikiana na wizara yake katika kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Zanzibar, Juma Malik Akili, amesema ziara hiyo imelenga kukagua maendeleo ya miradi iliyotengewa fedha katika mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema wizara yake imeridhishwa na hatua iliyofikiwa na sasa inaangalia maeneo mapya ya kuwekeza katika bajeti ijayo.
“Tunafarijika kuona miradi imefikia hatua nzuri. Wananchi waendelee kuwa wavumilivu, kwani maboresho makubwa yanakuja,” amesema.
Kwa sasa, Zanzibar inategemea kwa kiasi kikubwa chanzo kimoja cha umeme, hali inayochochea juhudi za Serikali za kupanua vyanzo vya uzalishaji ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa kudumu.