TRA yaja na utaratibu kudhibiti magendo mafuta ya kula

Dar es Salaam. Wakati malalamiko ya bei na upatikanaji wa mafuta ya kula yakiendelea kujitokeza mara kwa mara nchini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kuchukua hatua kudhibiti biashara ya bidhaa hiyo kwa kuanzisha utaratibu maalumu wa kuingiza mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

Hatua inayolenga kuziba mianya ya magendo na ukwepaji wa kodi, changamoto ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wamiliki wa viwanda vya mafuta hayo nchini.

Utaratibu huo, ambao unatarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni, pia unatajwa kuwa utasaidia kurahisisha biashara kati ya pande mbili za Muungano huku Serikali ikitarajia kuongeza mapato na kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha mafuta ya kula.

Akizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam na Zanzibar hivi karibuni, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema mamlaka hiyo imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mfumo huo mpya ili kuweka mazingira bora ya biashara ya mafuta ya kupikia.

Machi 25, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Mwenda alisema tayari hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kuunda kamati ndogo ya wataalamu.

Kamati hiyo inahusisha Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, maofisa wa forodha pamoja na waagizaji wa mafuta kwa lengo la kuweka utaratibu utakaoongoza uingizaji wa bidhaa hiyo.

Kwa mujibu wa Mwenda, mfumo huo mpya utasaidia kurasimisha biashara ya mafuta kati ya Zanzibar na Tanzania Bara na pia kuchochea shughuli za kiuchumi katika bandari ndogo zinazotumika kupokea mafuta hayo.

Bandari zinazotarajiwa kunufaika zaidi ni Bagamoyo, Mbweni na Kunduchi ambazo zimekuwa zikitumika kuingiza mafuta yanayotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

“Tutatoa punguzo kwa mafuta yanayoingia Tanzania Bara kutoka Zanzibar ili kuwawezesha wanaoingiza mafuta hayo kupata faida, Serikali ipate kodi na wakati huohuo kulinda viwanda vya ndani,” amesema Mwenda.

Amesisitiza kuwa pamoja na kuweka utaratibu huo, TRA haitasita kuchukua hatua kali kwa wafanyabiashara watakaoendelea kujihusisha na magendo ya mafuta ya kula.

“Hakuna atakayekuwa juu ya sheria. Baada ya kuanza kwa mfumo huu, yeyote atakayejihusisha na magendo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Hatuwezi kuacha biashara hii iendelee kama inavyofanyika sasa. Tutaweka utaratibu utakaowezesha uingizaji wa mafuta na kulinda viwanda vya ndani, ikiwemo kutoa punguzo la kodi ili wafanyabiashara wapate faida,” Mwenda.

Hatua hiyo inakuja wakati suala la mafuta ya kula limekuwa likizungumzwa mara kadhaa nchini kutokana na changamoto za uzalishaji wa ndani, utegemezi wa mafuta kutoka nje pamoja na hofu ya uwepo wa magendo yanayopunguza mapato ya Serikali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Ali Suleiman Ameir ameipongeza TRA kwa kuanzisha utaratibu huo akisema utasaidia kuweka uwazi katika biashara hiyo.

Amesema hatua hiyo pia itachochea ukuaji wa biashara na kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi zinazolipwa na wafanyabiashara.

Amesema ziara ya kamati hiyo ililenga pia kujifunza namna Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) unavyofanya kazi, akibainisha kuwa matumizi ya mfumo huo yamepunguza muda wa kupata huduma na kurahisisha mawasiliano kati ya walipakodi na TRA.