VIWANGO vizuri vinavyoonyeshwa na makipa watatu wa Azam, Aishi Manula, Zuberi Foba na Issa Fofana, vimempa matumaini makubwa ya kufanya vizuri kocha mkuu wa kikosi hicho, Mkongomani Florent Ibenge, katika michuano tofauti ya msimu huu.
Katika mechi 15 za Ligi Kuu Bara ilizocheza Azam msimu huu, Manula ndiye anayeongoza kwa kucheza nyingi zaidi, akifanya hivyo mara saba, akirejea katika kikosi hicho akitokea Simba baada ya kuondoka mwaka 2017.
Manula aliyeondoka Azam mwaka 2017, kisha kujiunga na Simba, amerejea ndani ya kikosi hicho msimu huu ambapo hadi sasa ana ‘Clean Sheets’ sita za Ligi Kuu Bara, katika mechi saba alizocheza.
Kwa upande wa Foba, amecheza mechi tano za Ligi Kuu Bara kati ya 15 za kikosi hicho msimu huu, ambapo nyota huyo hajaruhusu nyavu zake kutikiswa, akiwa na ‘Clean Sheets’ tano, akiendelea kuaminiwa hadi timu ya taifa ya Taifa Stars.
Naye Fofana, aliyejiunga na timu hiyo Agosti 15, 2025, akitokea Al-Hilal Omdurman ya Sudan aliyotokea pia Kocha, Ibenge kabla ya kutua Azam, amecheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara, huku kipa huyo akiwa na ‘Clean Sheets’ moja.
Akizungumzia viwango vya makipa hao, Ibenge alisema timu hiyo imefanya usajili mzuri wa nafasi pia mbalimbali uwanjani, hivyo jukumu lake ni kuhakikisha wachezaji wote wanakuwa na furaha, kwa kuwapa kila mmoja wao dakika kadhaa za kucheza. “Kila mmoja ana kitu cha kipekee, ila wote kwa pamoja ukiwaangalia wana uwezo unaofanana, ndio maana tunagawa baadhi ya mechi ili wacheze, sio eneo lao tu, kwa sababu hata nafasi nyingine pia uwanjani zina ushindani mkali,” alisema Ibenge.