Uchunguzi madai ya shule kuwa na kitabu kimoja wabaini siyo kweli

Rombo. Sakata la mama aliyejitokeza mbele ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akidai kuwa Shule ya Msingi Kirachi iliyopo Kata ya Kisale Msaranga, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, ina kitabu kimoja tu cha hisabati kwa darasa la saba, limechukua sura mpya baada ya uchunguzi kubaini kuwa taarifa hizo si za kweli.

Uchunguzi huo umeonyesha kuwa vitabu vya somo la hisabati katika darasa hilo vinatosheleza na vina uwiano unaokubalika kulingana na idadi ya wanafunzi.

Februari 19, 2026, Waziri Mkuu alipofanya ziara wilayani humo katika Kata ya Marangu Kitowo, mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Irene Kimario alikuwa miongoni mwa wananchi waliowasilisha kero zao, akitoa tuhuma hizo zilizozua taharuki miongoni mwa viongozi na wananchi.

Awali, Irene alidai kuwa shule hiyo ina upungufu mkubwa wa vitabu vya hisabati kiasi cha kuwa na kitabu kimoja tu kwa darasa zima, hali aliyosema inakwamisha wanafunzi kujifunza ipasavyo kulingana na malengo ya Serikali.

Akizungumza leo Machi 26, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amesema baada ya madai hayo, waliunda timu ya uchunguzi ili kubaini ukweli wa suala hilo.

 “Baada ya kupokea malalamiko hayo, tulituma timu kufanya uchunguzi wa kina. Matokeo yanaonyesha kuwa madai yaliyotolewa si ya kweli, kwani vitabu vya hisabati vinapatikana kwa uwiano unaokubalika shuleni hapo,” amesema Mwangwala.

Ameongeza kuwa hakuna upungufu wa vitabu kama ilivyodaiwa, na kusisitiza kuwa taarifa zilizotolewa awali zilikuwa na upotoshaji.

Aidha, mkuu huyo wa wilaya ameitaka jamii kuhakikisha wanawasilisha kero zenye ukweli wanapopata fursa ya kuzungumza na viongozi ili kuepuka kuleta taharuki isiyo ya lazima katika jamii.