******
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Jumla ya vijana 34 wanufaika wa mpango wa Samia Scholarship Extended DS/AI+ wanatarajiwa kupata punguzo la ada ya masomo kwa asilimia 50 katika Chuo Kikuu cha Limerick nchini Ireland, kufuatia makubaliano yaliyotiwa saini Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yamefikiwa kati ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na chuo hicho, yakilenga kupanua fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Kitanzania katika fani za kisasa zikiwemo Sayansi ya Data, Akili Unde na Sayansi Shirikishi.
Vijana hao ni sehemu ya wanufaika 50 wa mpango huo wa ufadhili unaolenga kukuza rasilimali watu wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya teknolojia.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda alisema mpango huo ni hatua muhimu katika kuwawezesha vijana wenye vipaji kupata elimu na ujuzi unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa ya kidijitali.
Alifafanua kuwa jitihada hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, inayosisitiza umuhimu wa kuimarisha masomo ya sayansi na teknolojia.
Kwa upande wake, Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan aliipongeza Tanzania kwa kuanzisha mpango huo, akieleza kuwa utanufaisha taifa kupitia vijana watakaorejea wakiwa na ujuzi na uzoefu utakaosaidia kukuza sekta za ubunifu na teknolojia.
Naye Makamu wa Rais wa Ushirikiano wa Kimataifa na Jamii wa chuo hicho, Colin Fitzpatrick alisema wanafunzi hao watanufaika na mazingira bora ya kujifunza pamoja na fursa za mafunzo ya vitendo kupitia ushirikiano wa chuo na makampuni makubwa ya kimataifa.
Alibainisha kuwa uzoefu huo utawasaidia wahitimu hao kuongeza ushindani wao katika soko la ajira la kimataifa.
.webp)
.webp)
.webp)
.webp)
.webp)
.webp)
.webp)
.webp)