Wanawake viongozi watajwa chachu ya ukuaji wa kampuni

Dar es Salaam. Maadili ya uongozi, uaminifu, uwezo wa kujali wafanyakazi na malezi bora vimetajwa kuwa miongoni mwa sifa muhimu zinazowafanya wanawake kuwa nguzo katika ufanisi wa taasisi na kampuni.

Wataalamu wanasema kuwapa wanawake nafasi za uongozi si tu kunaleta tija ya kijamii, bali pia kunachochea mafanikio ya kibiashara na kuimarisha mazingira rafiki ya kazi kwa wafanyakazi.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Machi 26, 2026, na Ofisa Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Emmanuel Nyalali, wakati wa warsha iliyoandaliwa na DSE kwa kushirikiana na Shirika la International Finance Corporation (IFC), mwanachama wa kundi la Benki ya Dunia.

Warsha hiyo imelenga kuhamasisha kampuni zilizoorodheshwa katika soko hilo pamoja na mawakala wake kuzingatia usawa wa kijinsia, ambao bado haujapewa kipaumbele cha kutosha katika baadhi ya taasisi.

Nyalali amesema kuwashirikisha wanawake katika nafasi za uongozi kunachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya taasisi kutokana na sifa walizonazo zinazojenga taswira ya uongozi bora.

β€œTunasisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake kuanzia ngazi za bodi hadi menejimenti, kwa kuwa mchango wao ni muhimu si tu kwa kampuni, bali pia kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,” amesema.

Ameongeza kuwa kuwapa wanawake nafasi kunasaidia kukuza biashara kwa sababu ya uwezo wao wa kujenga uaminifu na kuwajali wengine, sifa zinazochangiwa pia na majukumu yao ya malezi.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT), Said Kambi, amesema jitihada za kuwawezesha wanawake katika uongozi zinapaswa kuendeshwa kwa mikakati maalumu, badala ya kutegemea usawa wa kawaida pekee.

Amesema kuna umuhimu wa kuandaa kizazi cha wanawake watakaoweza kuingia katika nafasi za uongozi kwa kuwajengea uwezo na ujuzi unaohitajika.

β€œLengo si kugawana nafasi, bali kuwawezesha wanawake kwa kuwapa umahiri na kujenga utamaduni unaoruhusu kila mtu kuchangia mawazo na kushiriki kikamilifu,” amesema.

Ameongeza kuwa programu hizo zinapaswa kuhusisha ushirikiano na mashirika na kampuni mbalimbali, huku zikilenga pia kuwainua wanawake ili wasaidie wengine kufikia nafasi za juu.

Naye Mkurugenzi wa Hazina na Masoko ya Mitaji wa Benki ya CRDB, Alex Ngusaru, amesema bado kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa zaidi katika kuwawezesha wanawake, hususan katika kampuni zilizoorodheshwa DSE.

Amesema taasisi yao tayari imeanza kuchukua hatua kwa kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za juu za uongozi.

β€œProgramu hizi ni muhimu katika kufikia malengo ya kuwawezesha wanawake na kuhakikisha wanapata nafasi stahiki katika uongozi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Wafanyakazi na Masilahi katika kampuni ya Vodacom Tanzania, Gervas Mfugusa, amesema kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha wanawake, ikiwemo kuwajengea uwezo na kuwahamasisha kushika nafasi za uongozi.

Amesema jitihada hizo zimekuwa zikisaidia kuongeza uwakilishi wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi, jambo linalochangia ukuaji wa kampuni na ustawi wa wafanyakazi.