Dar es Salaam. Vikundi vya akiba na mikopo (Vicoba) katika wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro vimejiandaa kunufaika na fursa ya mikopo itakayotolewa na Taasisi ya fedha ya VisionFund Tanzania Microfinance Bank kwa kushirikiana na Norwegian Church Aid (NCA).
Mikopo hiyo ambayo ina riba ndogo, itawawezesha wanawake katika vikundi hivyo kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali na kufikia ndoto zao kupitia vipato watakavyojipatia kwenye shughuli hizo.
Matumaini ya wanawake hao yamechochewa na taasisi hizo kuanzisha mfuko wa mikopo wenye thamani ya Sh200 milioni, ukiwa na lengo la kupanua upatikanaji wa mikopo nafuu kwa makundi ambayo hayahudumiwi ipasavyo na taasisi za kifedha.
Kila taasisi imechangia kiasi sawa cha fedha huku zikichanganya rasilimali za kifedha na utaalamu wa uendeshaji ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo.
Katika ushirikiano huo, VisionFund itasimamia utoaji na uendeshaji wa mikopo, ikijumuisha tathmini ya wakopaji, utoaji wa fedha, ufuatiliaji na urejeshaji wa mikopo. Pia, matumizi ya mifumo ya kidijitali yamepangwa kuimarisha ufanisi na kupunguza vikwazo vya kiutendaji.
Kwa upande wake, NCA itatoa fedha kwa masharti nafuu, kubeba sehemu ya hasara inayoweza kujitokeza kupitia dhamana, pamoja na kugharamia ruzuku ya riba ili kuwawezesha wakopaji kupata mikopo kwa riba ya asilimia sita hadi tisa, ikilinganishwa na kiwango cha soko kinachofikia asilimia 21.
Mpango huo unalenga kukabiliana na changamoto za kimuundo katika sekta ya fedha nchini, ambapo wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) hukumbana na riba kubwa, masharti magumu ya dhamana na taratibu ndefu, hali inayowazuia kupata huduma za benki kwa urahisi.
Kupitia utoaji wa mikopo yenye riba ya chini ya tarakimu mbili, ushirikiano huo unajibu hitaji la haraka la upatikanaji wa fedha nafuu kwa wananchi wengi zaidi, huku ukichochea ujumuishwaji wa kifedha na kukuza uchumi endelevu nchini.
Changamoto za urejeshaji wa mikopo zitashughulikiwa kwanza na VisionFund, kabla ya dhamana ya NCA kuingilia kati kupunguza hasara zozote zitakazobaki.
Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, leo Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam, mratibu wa vikundi vya Vicoba vya Mvomero na Kilosa, Elizabeth Paskali amesema wanafarijika kuwa wanufaika wa Vision Fund kwani itakuwa ni mkombozi wao.
“Tunaumia sana kwa benki nyingine ambazo zinatoa mikopo kwa riba kubwa. Kwa kutumia benki hii, tutapiga hatua kubwa kwa sababu riba zao ni ndogo, hivyo tutapata faida katika shughuli zetu,” amesema Elizabeth.
Kwa upande wake, mmoja wa wanakikundi kutoka Mvomero, Lydia Buyonga amesema benki hiyo ambayo ina riba nafuu itawanufaisha kwa sababu wamekuwa wakikopa kwenye benki zile ambao zina riba kubwa, hivyo hawapati faida kwenye shughuli zao.
Awali, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika Dar es Salaam, leo Machi 26, 2026, Mkurugenzi Mkazi wa NCA, Berte Marie Ulveseter amesema:
“Ushirikiano huu unaonyesha namna juhudi za pamoja zinavyoweza kuleta matokeo chanya kwa kutoa suluhisho za kifedha nafuu kwa wanaozihitaji zaidi. Lengo letu ni kuziwezesha jamii huku tukihakikisha mfumo unabaki kuwa endelevu na wenye uwazi.”
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa VisionFund Tanzania, Deogratias Siria, amesema:
“Kupitia mpango huu wa pamoja, tunarahisisha upatikanaji wa mikopo kwa uwajibikaji. Kwa kuunganisha ufanisi wa kidijitali na msaada wa kifedha nafuu, tunaweza kuwasaidia wananchi kufikia malengo yao ya kifedha huku tukilinda ustawi wao wa muda mrefu.”
