LICHA ya kutofanya vizuri msimu huu katika kikosi cha Namungo FC, ‘Wauaji wa Kusini’, mshambuliaji wa timu hiyo, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ amesema bado ana vitu vingi vya kujifunza, kutoka kwa washambuliaji wenzake kikosini humo.
Nyota huyo anayefananishwa na mshambuliaji wa Manchester City ya England, Erling Braut Haaland, amekuwa na wakati mgumu tangu ajiunge na kikosi hicho Julai 21, 2025 akitokea TMA FC ya Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shahame, amesema ushindani wa nafasi katika eneo la ushambuliaji umekuwa mkubwa zaidi jambo linalosababisha kushindwa kupenya mara kwa mara kikosi cha kwanza, japo ni changamoto aliyoigeuza fursa maishani mwake.
“Siwezi kulaumu kwa sababu wenzangu wanafanya vizuri zaidi yangu, mazingira ya nilipotoka na hapa ni tofauti, bado nina muda wa kuendelea kushawishi benchi letu la ufundi, kwa kila nafasi nitakayopata uwanjani ya kucheza,” amesema Shahame.
Mshambuliaji huyo anasema uwepo wa washambuliaji wenzake, akiwemo Mkongomani, Fabrice Ngoy anayeongoza kwa sasa katika Ligi Kuu baada ya kufunga mabao manane, ni chachu zaidi ya kumpa motisha ya kupambania kikosi cha kwanza na kuonekana.
“Huu ni msimu wangu wa kwanza hapa Namungo na bado kuna nafasi nyingine ya kuendelea kuonyesha kipaji changu, unapokosa fursa ya kucheza mara kwa mara inaumiza mchezaji, ingawa kwangu nimechukulia kawaida na ninafurahia mazingira nilipo.”
Baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na TMA msimu wa 2024-2025, Shahame alisajiliwa na Namungo ili kuongezea nguvu katika eneo hilo la ushambuliaji, ingawa tangu amejiunga na kikosi hicho amefunga bao moja tu.
Bao hilo la Shahame aliifungia Namungo dakika ya 90+4, likiwa ni la kuchomoa katika sare ya 1-1 dhidi ya dhidi ya Pamba Jiji, Septemba 18, 2025.
Shahame aliyejiunga na TMA FC msimu wa 2022-2023, akitokea Pan Africans aliyoachana nayo pia akitokea Mbeya Kwanza, kwa msimu wa 2024-2025, aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Championship, baada ya mshambuliaji huyo kufunga mabao 18.
Mabao 18 aliyofunga Shahame, yaliwafanya washambuliaji watatu kuibuka wafungaji bora wakiwemo Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Andrew Simchimba aliyekuwa Geita Gold na sasa anaichezea Mtibwa Sugar kwa mkopo akitokea Singida Black Stars.
