Dar es Salaam
KAMPUNI ya Airtel Tanzania imezindua rasmi mnara wa mawasiliano wenye teknolojia ya 4G na 5G katika mtaa wa Machimbo, Tabata, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kuboresha huduma za mawasiliano na kukuza uchumi wa kidijitali kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Afisa Mtendaji wa Kata ya Machimbo, Bi. Lidya Bwathondi, alisema kuwa uwekezaji huo umeleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambao awali walikumbana na changamoto za mawasiliano.
“Kabla ya ujio wa mnara huu, wakazi wa Machimbo walikuwa wanapata shida kupata mawasiliano ya uhakika. Leo hii hali imebadilika, mawasiliano yameimarika na wananchi wanaweza pia kufanya biashara zao mtandaoni kwa urahisi zaidi,” alisema Bwathondi.
Kwa upande wake, Meneja Biashara wa Airtel, Bw. Benson Mbwanga, alieleza kuwa uzinduzi wa mnara huo ni sehemu ya mkakati wa Airtel wa kuendelea kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini.
“Uwekezaji huu unaonesha dhamira ya Airtel ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za mawasiliano. Tunaendelea kupanua mtandao wetu wa 4G ili kuwezesha wananchi kuwasiliana kwa urahisi, kufanya biashara za kidijitali na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa,” alisema Mbwanga.
Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Machimbo, akiwemo Bi. Mariam Simon, Bi. Bertha Livingston, Bi. Khadija Seif na Bi. Sada Nyambe, walieleza kufurahishwa kwao na uwekezaji huo wakisema utarahisisha shughuli zao za kila siku, hususan biashara za kidijitali, na kuishukuru Airtel kwa kuchagua kuwekeza katika eneo lao.
Uzinduzi wa mnara huu ni sehemu ya uwekezaji mpana wa Airtel ambapo jumla ya minara mipya tisa yenye teknolojia ya 4G imejengwa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni jitihada za kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano na kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Airtel Tanzania inaendelea kujikita katika kutoa huduma bora, za uhakika na zenye ubunifu, huku ikiunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano bora kwa Watanzania wote.

