Hakimu Hellerstein Kusikiliza Pingamizi la Kisheria la Maduro

Global Publishers
March 27, 2026
0 Comments

Rais wa zamani wa Venezuela, Nicolás Maduro.

New York, Marekani – Rais wa zamani wa Venezuela, Nicolás Maduro, kurejea mahakamani leo Alhamisi 27, 2026 mjini New York huku akihoji uhalali wa mashtaka ya dawa za kulevya yanayomkabili.

Maduro pamoja na wakewe, Cilia Flores, watakuwa mahakamani kwa mara ya kwanza tangu kesi yao ilipoanza Januari, pale ambapo Maduro alikataa mashtaka dhidi yake na kusema: “Sijawahi kufanya kosa. Mimi ni mtu mwema, Rais wa kikatiba wa nchi yangu.” Flores pia amekataa mashtaka yote.

Wote wanashikiliwa katika katika Gereza la Brooklyn linalojulikana kama Metropolitan Detention Center (MDC) na hawajaomba dhamana. Hakimu Alvin Hellerstein bado hajapanga tarehe ya kuanza kwa kesi, ingawa jambo hilo linaweza kujadiliwa katika kikao hiki cha mahakama.

Maduro anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika usafirishaji wa cocaine na ugaidi wa dawa za kulevya, yaliyokuwa yamefungwa kisheria na kisha kufunguliwa upya baada ya kukamatwa Januari.

Moja ya hoja kuu katika mahakama ni iwapo serikali ya Venezuela inaruhusiwa kufadhili utetezi wa kisheria wa Maduro, jambo ambalo wanasheria wake wanasema linakiuka haki yake ya kupata utetezi huru kutokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya matumizi ya rasilimali za serikali.