Jumanne Challe aanika ‘mchawi’ KenGold, akiri ugumu wa kurejea Ligi Kuu

KOCHA Mkuu wa KenGold, Jumanne Challe, amesema kukosa balansi katika eneo la kujilinda na ushambuliaji ndio sababu kubwa ya kikosi hicho kutokuwa na mwenendo mzuri msimu huu, japo, anaridhishwa na maendeleo ya mchezaji mmoja mmoja kikosini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Challe, amesema malengo yao mwanzoni yalikuwa ni kumaliza nafasi nne za juu, ingawa, kwa hali ilivyo na mwenendo wa timu hiyo ni ngumu kufikia kile walichokusudia, japo, wataendelea kupambana kwa mechi tisa zijazo.

“Ushindani na wapinzani wetu ni mkubwa sana na hata ukiangalia gepu la pointi unaona ni ngumu kuwafikia, japo hatujakata tamaa, kwa sababu mechi hizo tisa zilizobakia ambazo ni sawa na pointi 27, lolote linaweza kutokea pia,” amesema Challe.

Kocha huyo amesema hali hiyo imechangia kurudisha nyuma maendeleo ya kikosi hicho msimu huu, ingawa anaendelea kupambana kwa mechi zilizobakia, hususani kutengeneza balansi nzuri kwenye eneo la kujilinda ambalo ndilo limekuwa ni changamoto.

Baada ya msimu bora wa 2023-2024, mashabiki na wapenzi wa soka hususani wa jijini Mbeya walitarajia KenGold ingeendeleza ilichokifanya katika Ligi ya Championship, japo, baada ya kupanda daraja mambo yalikuwa ni tofauti na kurejea ilipotoka.

Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.

Licha ya kiwango bora, ila KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu, ambapo msimu wa 2024-2025, iliburuza mkiani na pointi 16, ikishinda mechi tatu tu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza ya 15 na pointi 23.

Kwa msimu huu wa 2025-2026, KenGold imeshinda mechi saba tu, ikitoka sare tano na kupoteza tisa kati ya 21, ikiwa nafasi ya nane na pointi 26, huku safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ikifunga mabao 21 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 23.