Dar es Salaam. Wadau wa teknolojia ya fedha (fintech) Afrika Mashariki wamesema mustakabali wa sekta hiyo haupo tena katika kuongeza ufikiaji wa watu wengi, bali katika kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaleta matokeo ya kiuchumi yanayopimika kwa watu binafsi na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa huduma za fedha kidijitali zimefikia asilimia 90 hadi 95 ya wananchi katika baadhi ya maeneo ya ukanda huo, lakini wadau wanasema jambo la msingi sasa ni kuhakikisha huduma hizo zinachangia moja kwa moja kuboresha maisha ya watu.
Akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji Afrika Mashariki 2026, lililoanza Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Huduma za Kifedha na Ujumuishaji katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kennedy Komba alisema mafanikio ya sekta hiyo yanapaswa kupimwa kwa matokeo halisi badala ya idadi ya watumiaji.
“Swali muhimu sasa siyo tena kama watu wanaweza kupata huduma hizi, bali ni kama zinaboresha maisha yao ya kila siku,” alisema Komba.
Alisema sekta inapaswa kuongeza thamani yake kwa kusaidia biashara ndogo, kusaidia kaya kukabiliana na changamoto za kifedha na kuimarisha uthabiti wa kifedha wa muda mrefu.
Pili, alisisitiza umuhimu wa kurejesha imani ya watumiaji, akibainisha kuwa wasiwasi kuhusu udanganyifu, tozo zisizo wazi na mikopo ya kidijitali yenye masharti kandamizi vimepunguza imani hiyo.
Alisema udhibiti madhubuti, uwazi wa gharama, na kuimarisha elimu ya fedha vitakuwa muhimu katika kurejesha imani na kuhamasisha matumizi endelevu.
Tatu, alitoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda, akieleza kuwa tofauti za mifumo ya udhibiti na ukosefu wa mwingiliano wa mifumo ni vikwazo kwa biashara na uwekezaji wa mipakani.
“Kuunganisha kanuni za udhibiti, kuwekeza katika miundombinu ya pamoja ya kidijitali, na kuboresha mifumo ya malipo kutakuwa muhimu katika kufungua uwezo kamili wa Fintech Afrika Mashariki,” alisema.
Komba aliongeza kuwa licha ya ukanda huu kuweka msingi imara wa mfumo wa kifedha wa kidijitali, hatua inayofuata inahitaji kuunganisha mifumo hiyo katika mtandao mmoja ulioratibiwa unaoweza kusaidia biashara, uimara wa uchumi, na ustawi wa pamoja.
Akisisitiza umuhimu wa ushirikiano, Mwenyekiti wa Shirikisho la Fintech Tanzania (Tafina), Cynthia Ponera alisema ubia utakuwa nguzo kuu ya kuamua mustakabali wa sekta hiyo.
“Wadau wanapaswa kwenda zaidi ya kutoa fedha na kuwa washirika halisi katika kuendesha ubunifu na mijadala. Hii ndiyo itakayofungua hatua inayofuata ya ukuaji wa uchumi wa ukanda wetu,” alisema.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya kongamano hilo, Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, Zuwena Farah, alisisitiza umuhimu wa miundombinu na sera rafiki katika kudumisha uchumi wa kidijitali.
Alionya dhidi ya utozaji kodi kubwa kupita kiasi kwa sekta hiyo, akiwahimiza watunga sera kuilea kama kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi.
“Miundombinu ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa kidijitali. Minara tunayojenga, nyaya za mawasiliano tunazoweka, vituo vya data, majukwaa ya kompyuta mtandao (cloud) na mifumo ya malipo, hivi vyote ni barabara na madaraja ya karne ya 21,” alisema.
Akirejea historia ya huduma za fedha kwa simu, alitaja uzinduzi wa M-Pesa takribani miongo miwili iliyopita kuwa hatua muhimu iliyoonyesha nguvu ya teknolojia yenye malengo mahsusi.
Alisema kwa sasa, malengo yamepanuka zaidi ya upatikanaji wa huduma, huku waendeshaji wakilenga kuleta mageuzi ya kiuchumi yenye maana katika ukanda mzima.
