Kisa Simba, Yanga, TFF yatoa siku 60

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa notisi ya kisheria ya siku 60 kwa kampuni kadhaa za ubashiri, ikizitaka zitoe maelezo kwa nini zisichukuliwe hatua za kisheria kwa kuorodhesha mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Yanga dhidi ya Simba kwenye majukwaa yao bila idhini.

Mechi hiyo iliyochezwa Machi 1, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ilimalizika kwa timu hizo kutofungana. Hata hivyo, matukio ya nje ya uwanja ndiyo yamezua mjadala mkubwa, huku TFF ikizishutumu baadhi ya kampuni za kubashiri kwa kukiuka kanuni zilizowekwa.

Kabla ya mechi hiyo, TFF ilikuwa imetangaza rasmi fursa kwa kampuni za kubashiri kuwasilisha maombi ya kupata kibali cha kujumuisha mchezo huo kwenye majukwaa yao.

Katika taarifa iliyotolewa Februari 18, 2026, shirikisho hilo lilieleza wazi kwamba lilikuwa na nia ya kutoa haki ya kipekee ya kubashiri kwa kampuni moja tu. Taarifa hiyo pia ilitoa onyo kali kwamba kampuni yoyote itakayokiuka agizo hilo itachukuliwa hatua za kisheria.

TFF ilisisitiza kuwa, zuio hilo halikuhusu tu mechi ya Yanga dhidi ya Simba, bali lilihusu pia mechi zote za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine yote yaliyo chini ya mamlaka yake.

Licha ya maelekezo hayo, baadhi ya kampuni zinadaiwa kupuuza utaratibu huo na kuendelea kuorodhesha mechi hiyo kwa ajili ya kubashiri bila idhini.

Shirikisho hilo lilisema vitendo vya kampuni hizo vinakiuka maelekezo yake na vinakwenda kinyume na maslahi ya soka la Tanzania.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura alithibitisha kuwa shirikisho limebaini ukiukwaji kadhaa. Alieleza kuwa, licha ya TFF kuweka utaratibu wazi na wa haki kwa kampuni za kubashiri kuomba haki hizo, baadhi ya kampuni zilichagua kutofuata taratibu zilizowekwa.

Wambura amesema kuorodhesha mechi bila idhini ni ukiukwaji wa moja kwa moja wa kanuni za TFF, ambazo zinatambua shirikisho hilo kama msimamizi halali wa shughuli za soka nchini Tanzania. Kabla ya kuanza rasmi hatua za kisheria, TFF iliamua kutoa notisi ya siku 60 ili kutoa nafasi kwa kampuni husika kujieleza.

Inaelezwa kwamba, mechi ya Yanga dhidi ya Simba ni miongoni mwa zinazovutia zaidi, ikivuta kiasi kikubwa cha fedha za ubashiri kinachofikia mabilioni ya shilingi.

“Lengo la notisi hii ni kuzipa kampuni husika fursa ya kueleza kwa nini zilikiuka kanuni za TFF, ambazo zinasimamia soka nchini Tanzania,” amesema Wambura.

“Majibu yao yatatusaidia kuamua hatua sahihi za kisheria zitakazochukuliwa.”

Alipoulizwa kama notisi hiyo inajumuisha madai ya fidia au hasara, Wambura alikataa kutoa maelezo zaidi, akisema masuala hayo yatawekwa wazi baada ya kipindi cha notisi kumalizika.

“Hakuna haja ya kuingia kwa undani zaidi kwa sasa,” amesema na kuongeza:

“Kilicho wazi ni kwamba kampuni zilizokiuka taratibu zimepokea notisi ya kisheria. Hii ni hatua halali, na tunawaomba wananchi wawe na subira wakati mchakato huu unaendelea.”

Alisisitiza kuwa, kampuni zote za kubashiri lazima zifuate kikamilifu kanuni za TFF zinaposhughulika na mechi za soka zilizo chini ya mamlaka yake.

Kulingana naye, hakuna mechi yoyote ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara au mashindano mengine chini ya TFF inayopaswa kuwekwa kwenye majukwaa ya ubashiri bila kufuata taratibu sahihi za kupata idhini.

Hatua hii inaonesha msimamo thabiti wa TFF katika kulinda haki zake za kibiashara na kuhakikisha wadau wote wanafanya kazi ndani ya mfumo wa kisheria uliowekwa.