Kukosekana kwa wakalimani wa lugha za alama kikwazo kwa walemavu

Kahama. Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata) wilayani Kahama mkoani Shinyanga, limeeleza kuwa kukosekana kwa wakalimani wa lugha za alama katika ofisi za umma ikiwemo hospitali, mahakamani, vituo vya polisi na halmashauri bado ni kikwazo cha upatikanaji wa huduma sahihi kwa wenye uziwi.

Shirikisho hilo lenye jumla ya wanachama 3268, limeeleza kuwa hali hiyo hususani katika vituo vya kutolea huduma za afya, kunasababisha kundi hilo la jamii kupatiwa matibabu kwa kukisia ugonjwa kutokana na mgonjwa kushindwa kuelewana lugha na mtoa huduma.

Katibu wa Shivyawata wilayani humo Charles Kafuku, amebainisha hayo leo Machi 27, 2026 wakati wa mkutano wa katibu wa Nec, siasa na uhusiano wa kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, uliolenga kusikiliza na kutatua kero za makundi mbalimbali wilayani humo.

“Watu wenye uziwi, anapofika hospitali na hakuna mkalimani wake, inamletea shida daktari aliyepo zamu kumuelewa mgonjwa hivyo anabuni tu kile anachojieleza mgonjwa kwamba huyu inawezekana anasumbuliwa na malaria, kumbe hamna, sisi wenye ulemavu bado tunaona hatujatendewa haki.” Amesema Kafuku.

Aidha ameeleza kuwa mazingira ya kujifungua kwa watu wenye ulemavu sio rafiki na yanatweza utu wa wanawake wenye ulemavu, kwa kukosekana usiri wa kutosha na miundombinu ya ndani iliyo rafiki ikiwemo vitanda.

Amesema “Wanawake wenye ulemavu hawana mazingira rafiki ya kujifungua wanapofika hospitali, mfano vitanda ni vilevile vya wasio na ulemavu, usiri wa kujifungua hakuna na huku kwenye jamii yetu bado kuna tabia ya kuwashangaa wenye ulemavu, wanajikuta wanakosa furaha.”

Katibu wa Nec, siasa na uhusiano ya kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid amekiri kuipokea taarifa ya Shivyawata na kuahidi kuifikisha kwenye ngazi zinazohusika ili kuhakikisha sauti za wananchi hao zinasikika na kuzingatiwa katika ngazi za maamuzi.

Amesema serikali inatambua kundi la watu wenye ulemavu, imeboresha huduma katika maeneo mengi,  huku viti vya uwakilishi wa kundi hilo bungeni ukiongezeka kutoka viti viwili hadi vinne katika bunge la 13.

Amesema “Hoja zote zilizowasilishwa hapa zina mashiko na zinalenga kuboresha sera na sheria kwa manufaa ya jamii nzima, na mimi nawaahidi nitazibeba kama zilivyo. Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya makundi yote ya jamii hususani wenye ulemavu.”

Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu ambapo hivi karibuni imewajengea uwezo watendaji wake wa kutumia mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa unaojulikana kama PD-MIS.

Mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Ruvuma yalihudhuriwa pia na mwakilishi kutoka ofisi ya waziri mkuu Jackobo Mwinula aliyeeleza kuwa mfumo huo utawezesha watu wenye ulemavu kusajiliwa, kupata namba za utambulisho na kufikia huduma muhimu za kijamii kwa urahisi.