Dar es Salaam. Kila mara mwananchi anapoingia katika kituo cha afya au hospitali ya umma na kuambiwa dawa zimeisha, maswali huanza kumiminika akilini.
Miongoni mwa maswali hayo ni nani ameshindwa kutekeleza wajibu wake? Je, tatizo ni ukosefu wa fedha, uzembe wa watendaji au mfumo wenyewe una mapungufu?
Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dodoma hivi karibuni, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi anaeleza kwa kina namna mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, zikiwemo dawa, unavyofanya kazi na wapi hasa mambo yanaweza kwenda kombo.
Safari ya dawa inaanzia zahanati
Kwa mujibu wa Msasi, upatikanaji wa dawa hauanzii Wizara ya Afya wala Bohari ya Dawa (MSD), bali huanzia kwenye kituo cha afya chenyewe.
Kila mwaka, vituo vyote vya afya zaidi ya 8,000 nchini huanza mchakato wa kuandaa maoteo ya dawa kuanzia Agosti mosi hadi Desemba 31.
Katika kipindi hiki cha miezi minne, wahudumu wa afya hukusanya takwimu za wagonjwa, mwenendo wa magonjwa na matumizi ya dawa ili kubaini mahitaji yao ya mwaka unaofuata.
“Mfumo huu unatumia teknolojia ya kisasa inayoitwa Electronic Logistics Management Information System (eLMIS), ambapo vituo vyote vinaunganishwa na kuwasilisha mahitaji yake kwa njia ya kidigitali,” anaeleza Msasi.
Anasema hakuna kituo kinachoruhusiwa kuwasilisha mahitaji nje ya mfumo huo, hatua inayolenga kuongeza uwazi na ufuatiliaji.
Lakini hapa ndipo swali la kwanza linapoibuka: Je, wahudumu wa afya katika ngazi ya chini wana uwezo wa kufanya maoteo sahihi ya mahitaji ya dawa?
Msasi anasema baada ya vituo kuwasilisha maoteo yake, taarifa hizo hupitia hatua kadhaa za uchambuzi kuanzia halmashauri, mkoa hadi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katika kila ngazi, maoteo hayo huchujwa, kurekebishwa na kulinganishwa na vyanzo vya fedha vilivyopo. Mwisho wa mchakato huo, maoteo huwasilishwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Maoteo ya Dawa, inayoongozwa na Mfamasia Mkuu wa Serikali.
“Tunapokea mahitaji ya nchi nzima, tunayachambua na kuhakikisha yanaendana na uhalisia kabla ya kuyapeleka MSD kwa ajili ya utekelezaji,” anasema.
Hata hivyo, uwepo wa hatua nyingi za uchujaji unaibua hoja nyingine: Je, kuna uwezekano wa mahitaji halisi kupotea njiani au kubadilishwa kiasi cha kuathiri upatikanaji wa dawa?
Baada ya matokeo kupitishwa, hatua inayofuata ni upangaji wa ununuzi na usambazaji wa dawa (supply planning), unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Tamisemi na MSD.
Katika hatua hii, huangaliwa kiasi cha dawa kilichopo kwenye maghala na kile kinachohitajika kununuliwa ili kukidhi mahitaji ya mwaka mzima.
Lakini changamoto kubwa hujitokeza pale ambapo fedha zilizopo hazilingani na mahitaji yaliyobainishwa.
“Ikitokea kuna tofauti kati ya fedha na mahitaji halisi, hapo ndipo chanzo kingine cha upungufu wa dawa kinaanzia,” anabainisha Msasi.
Baada ya fedha kupatikana na dawa kununuliwa, jukumu la MSD ni kuhakikisha dawa zinafika katika vituo vya kutolea huduma kulingana na oda zinazowasilishwa kila baada ya miezi miwili.
Kwa upande wake, kituo cha afya kina wajibu wa kuagiza dawa kwa wakati na kwa usahihi kulingana na mahitaji yake.
Iwapo MSD itashindwa kutimiza oda, lawama huangukia kwake. Lakini kama kituo hakikuagiza ipasavyo au kilifanya makosa katika maoteo, uwajibikaji hurudi kwa wahudumu wa kituo husika na mamlaka za halmashauri.
“Huu ni mnyororo unaohusisha watu wengi, na kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake,” anasisitiza Msasi.
Hata hivyo kwa mtu wa kawaida, maelezo haya yanaweza yasitoshe. Swali lake huenda likabaki lile lile, kwa nini dawa haipo?
Ili kuondokana na changamoto hizo, Serikali imewekeza katika mifumo ya kidigitali ili kuboresha ufuatiliaji wa dawa. Mbali na eLMIS, pia kuna mifumo ya taarifa za wagonjwa (medical records) inayotumika katika vituo vya afya.
Lengo ni kuunganisha mifumo hiyo ili iweze kutoa taarifa kwa wakati, kuanzia dawa ilipoingia hadi ilipotolewa kwa mgonjwa.
“Tunalenga kufika mahali ambapo ndani ya dakika chache tunaweza kujua ni kituo gani kina uhaba wa dawa na kuchukua hatua haraka,” anasema Msasi.
Aidha, matumizi ya teknolojia ya akili bandia (Artificial Intelligence) yameanza kusaidia katika kufanya maoteo kwa usahihi zaidi.
Licha ya maelezo haya, bado kuna swali, je, teknolojia pekee inaweza kutatua changamoto za msingi kama uhaba wa wataalamu na rasilimali fedha bado ni hoja inayoibuka.
Moja ya changamoto kubwa inayokabili sekta ya afya ni uhaba wa wataalamu, hususan wafamasia.
Kutokana na hali hiyo, mara nyingi kazi za kupanga na kusimamia dawa hufanywa na wauguzi au wataalamu wa maabara, jambo linaloweza kuathiri ubora wa maamuzi.
Msasi anasema Serikali imeanza kuchukua hatua, ikiwemo kuajiri watumishi 12,000 katika sekta ya afya mwaka huu wa fedha.
“Kingine tunatoa sana mafunzo kwa wataalamu, watu wetu wapo field kutoa mafunzo, unamkuta nesi au mtaalamu wa maabara yupo pale, inabidi yeye atusaidie sisi katika kutengeneza maoteo na kufanya uhakiki wa dawa.
“Tuna imani ukiwa na wataalamu sahihi wakiwa wamekaa pale kama ambavyo Serikali inaendelea kulifanyia kazi, linaweza kuwa sukuhisho zuri zaidi kupunguza kero hii,” anasema Msasi.
Pamoja na juhudi zote, bado kuna changamoto ya dawa kuharibika kutokana na kuisha muda wake wa matumizi.
Kwa mujibu wa Msasi, hali hii haiwezi kuepukika kabisa, hasa katika nchi zinazotegemea uagizaji wa dawa kutoka nje.
“Unalazimika kujiandaa kwa magonjwa hata kama hayatatokea. Yasipotokea, dawa zinabaki na kuharibika,” anafafanua.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa kipimo cha ufanisi ni kiwango cha dawa kinachoharibika. Kwa sasa, Tanzania ipo chini ya asilimia mbili wakati kiwango cha kimataifa ni asilimia tano.
“Tunachokipima duniani ni asilimia ya dawa zilizoharibika ukilinganisha na kiwango ambacho ulikinunua ukakiingiza nchini kwa wakati huo, sisi mwaka wa fedha ulioisha 2024/2025 dawa ambazo tumekuta zimeharibika ni kama asilimia 0.9, hata asilimia 2 kiwango ambacho tulikiona huko nyuma ndani ya nchi hakikufika,” anasema Msasi.
Lakini kwa macho ya mwananchi, hata kiwango hicho kinaweza kuonekana kikubwa, hasa pale anapokosa dawa hospitalini.
“Dawa kuchina kwenye kituo au ghala la MSD ni jambo lisiloepukika maana tunanunua na kusubiri magonjwa, kama kipindupindu hakikutokea dawa zitaharibika,” anasema Msasi.
Msasi anasema mbali na changamoto za mifumo na fedha, pia kuna tatizo la uchepushaji wa dawa.
Ripoti mbalimbali zimekuwa zikionyesha kuwepo kwa vitendo vya wizi na ubadhirifu wa dawa, huku baadhi ya watumishi wakichukuliwa hatua za kisheria.
Msasi anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo, lakini anasema kuna mifumo madhubuti ya ufuatiliaji, ikiwemo ukaguzi wa ndani na nje, pamoja na ushirikiano na vyombo kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambambana na Rushwa (Takukuru).
“Tukigundua dawa hazikufika kwa mgonjwa, zimechepushwa, taarifa huwa inaanza kupanda kwenye vitengo na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, CAG anaweka kwenye ripoti na tunachukua hatua,” anasema na kuongeza:
“Kama mnafuatilia kuna kesi za watumishi ziko mahakamani, kuna watu walitaifisha vifaa tiba, wengine dawa. Wengine wakifungwa na wengine wanachukuliwa hatua, kuna taarifa mbalimbali, kuna kesi nyingi zinatokea wenzetu Takukuru wanafanya kazi maalumu kuhakikisha kuna ufuatiliaji na bidhaa za afya hazichepushwi.”
Msasi anasema katika mazingira ambayo dawa zinakosekana kwenye vituo vya umma, mwananchi hulazimika kununua dawa katika vituo binafsi kwa gharama zake mwenyewe.
Hali hii inaongeza mzigo wa kifedha kwa wananchi, hasa wale wa kipato cha chini.
Serikali ina matumaini kuwa utekelezaji wa bima ya afya kwa wote utasaidia kupunguza tatizo hili, kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bila kulazimika kutoa fedha mfukoni.
Kwa mtazamo wa kina, ni wazi kuwa hakuna jibu rahisi kuhusu nani wa kulaumiwa pale dawa zinapokosekana.
Ni mnyororo mrefu unaohusisha wahudumu wa afya, halmashauri, mikoa, Wizara ya Afya, MSD na hata Wizara ya Fedha.
Hata hivyo Msasi anasema kila kiungo kinaposhindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, athari yake huonekana kwa mtu wa mwisho anayehitaji huduma.
Lakini labda swali muhimu zaidi halipaswi kuwa nani wa kulaumiwa, bali ni jinsi gani mfumo huu unaweza kuboreshwa ili kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote.
