Lukuvi aagwa bungeni, wabunge watoboa siri

Dodoma. Ni mara chache kumuona Waziri William Lukuvi enzi za uhai wake akiingia Bungeni kwa kupanda gari, mara nyingi alitembelea na kutaniana na wenzake ilikuwa jadi yake.

Leo imekuwa kinyume chake, ameingia viwanja vya Bunge akiwa ndani ya sanduku, haongei, hajui akina nani wamehudhuria hapo lakini utani umekosekana pamoja na uwepo wake.

Lukuvi alifariki asubuhi ya Machi 25,2026 katika Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata mshituko wa moyo.

Mwili wa William Lukuvi umeingia huku kukiwa na utulivu uliopitiliza, watu wamevalia mavazi meusi kama waliokubaliana huku wachache wakivalia mavazi yenye rangi nyeupe na wachache kabisa walivaa nguo za kawaida ama sare za kazini ikiwepo watu wa ulinzi na viongozi wa dini.

Hata hivyo, mambo matano yaliyotajwa kuhusu Lukuvi yanaonyesha wazi alikuwa mtu wa namna yake ndani ya Taifa.

Viongozi mbalimbali wakiwa katika viwanja vya Bunge, Dodoma wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi.

Miongoni mwa hayo ni ushiriki wake katika ujenzi wa ukumbi mpya wa Bunge, usimamizi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), usimamizi wa ujenzi wa mji wa Serikali (Mtumba) na ubunifu kwa magari ya wanafunzi Jijini Dar es Salaam.

Mambo mengine ya kukumbukwa akiwa Wizara ya Ardhi ni zaidi ya miliki 1,992,245 alizotoa kwa Watanzania na kutenga ekari 224,439.4 kwa ajili ya uwekezaji.

Akisoma wasifu wa Marehemu mbele ya wabunge na wananchi Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jimi Yonaza amemtaja Lukuvi kama kioo na nembo kwa wabunge na mawaziri.

Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Marehemu, William Lukuvi likiwasili katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Yonazi amesema katika kipindi cha uhai wake, Lukuvi alipita katika nafasi mbalimbali za uongozi lakini Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu akishughulikia Bunge, Sera na Uratibu ndiyo iliyomtambulisha zaidi kwani alihudumu kwa mihula mitatu kwa nyakati tofauti.

Spika Mstaafu Dk Tulia Ackson amesema kuwa Lukuvi hakuwa mchoyo wa maarifa na watu wengi akiwemo yeye (Tulia) walijifunza vitu vingi kutoka kwake hoja ambayo iliibua shangwe ya makofi kutoka kwa waombolezaji.

“Alikuwa Mwalimu kuhusiana na siasa safi, kutokuwa mwizi, kuwa Mbunge Bora lakini hakufurahia kuona mtu alipatwa na mabaya,” amesema Dk Tulia.

Makamu wa Rais Mstaafu Dk Philip Mpango amesema katika kipindi cha uongozi wao, walimtumia Lukuvi kwa ajili ya kuwafunda Mawaziri na wabunge katika kutekeleza majukumu yao.

“Kuna wakati vyuma vilikuwa vimebana nilikuta na Mheshimiwa Lukuvi akasema sijawahi kukutana na Waziri wa fedha bahili kama wewe,” amesema Dk Mpango huku akikumbuka namna alivyomsaidia na kumwelekeza taratibu za Serikali ndani ya mjengo.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amesema katika kipindi cha uhai wake, William Lukuvi alikuwa mtuliza joto wakati linapopanda Bungeni.

Waziri Mkuu amesema kifo cha Mbunge huyo wa Isimani kimekuja wakati alishajenga imani kwake kama msaidizi ambapo alianza kuona kazi ya Waziri Mkuu ni nyepesi kwani kila wakati alimrahisishia kumudu majukumu yake vema.

Dk Mwigulu amesema, Marehemu atakumbukwa kwa mengi katika nchi ikiwemo kuwa na Utumishi uliotukuka, busara, ushawishi wake, weledi katika kazi, uzalendo, Uratibu ndani ya Bunge na mlezi wa kila mmoja.

Mdogo wa marehemu, Mosi Lukuvi amemtaja kaka yake kuwa alikuwa nguzo imara katika familia yao na wananchi wa Jimbo la Isimani alikokuwa mwakilishi wao kwa zaidi ya miaka 30.

Mosi pia amemuombea msamaha kaka yake akieleza kwenye mambo ya siasa kuna mapito mengi kwamba huenda aliwahi kukwazana na wenzake hivyo akasema kama yupo wa aina hiyo wanaomba msamaha kwa niaba yake na kwa waliomkosea akatoa msamaha kwao.

Mbunge wa Nzenga Mjini, Hussein Bashe amesema kilichokuwa kikimsaidia Lukuvi hata bajeti zake kupita bila kupingwa ni kwa sababu ya heshima aliyokuwa amejijengea kwenye mhimili.

Bashe amesema Lukuvi alikuwa amejijengea mahusiano mazuri pia hata kwa wabunge vijana ambao walikuwa na mihemko lakini alikuwa karibu nao na hivyo wakajenga heshima kwake.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde ametaja kilichombeba hata kuwa mtuliza joto bungeni ni kwamba aliipenda kazi yake na kujua na ndiyo maana alifanikiwa kwa kila jambo alilolifanya bungeni.

Kwa upande wake Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema Lukuvi alikuwa mfano mzuri kwa viongozi vijana kutokana na heshima aliyokuwa amejiwekea ya kufanya kazi kwa bidii kwani hakuwa mbovu.

Nape amesema kitendo hicho kilipelekea kuaminiwa Bungeni kwa kila alipokuwa akilisema ilikuwa lazima aungwe mkono na wabunge wote ikiwemo wa upinzani.