Magereza: Wafungwa waongezeka nchini, mahabusu wakipungua

Dar es Salaam. Takwimu mpya zilizotolewa na Jeshi la Magereza jijini Dodoma zimeonyesha mwelekeo mpya katika mfumo wa haki jinai nchini ambapo idadi ya mahabusu imepungua kwa kiwango kikubwa huku wafungwa wakiongezeka.

Akizungumza leo Machi 27, 2027 wakati wa uwasilishaji wa takwimu za wafungwa na mahabusi za mwaka 2025, Naibu Kamishna Msaidizi wa Magereza, Justine Kazulaya amesema mabadiliko hayo yanaonyesha mageuzi katika uendeshaji wa kesi na mifumo ya utoaji haki.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mwaka 2025, jumla ya wahalifu waliokuwapo magerezani walikuwa 23,940, ambapo wafungwa walikuwa 19,646 na mahabusu 4,294, hali hii ni tofauti na mwaka 2024 ambapo walikuwapo wahalifu 26,596, wafungwa 18,992 na mahabusu 4,294.

Amesema mabadiliko hayo yanaonyesha kupungua kwa uhalifu kwa asilimia 10, ongezeko la wafungwa kwa asilimia 3.6, huku mahabusu wakipungua kwa asilimia 43.8.

Kazulaya amesema takwimu hizo zinaonyesha wanaume ndio wanaounda idadi kubwa ya wahalifu kwa asilimia 97, huku wanawake wakiwa asilimia tatu pekee.

Kazulaya amesema si wahalifu wote wanapaswa kubaki mahabusu, jambo lililosababisha mwaka 2025 kuachiwa wafungwa 27,191 na mahabusu 27,426, ikilinganishwa na wafungwa 26,519 na mahabusu 25,444 mwaka 2024.

“Kupungua kwa mahabusu kunachangiwa na matumizi ya mahakama za mtandao, hatua iliyoharakisha usikilizwaji wa kesi kwa kushirikiana na vyombo vya uendeshaji mashtaka, mahakama na Jeshi la Magereza,” amesema Kazulaya.

Kwa upande mwingine, waliobadilika kutoka mahabusu kuwa wafungwa walikuwa 4,180 mwaka 2025, wakishuka kutoka 7,155 mwaka 2024, sawa na upungufu wa asilimia 41.6.

Kijiografia, mikoa inayoongoza kwa kuwa na wahalifu wengi ni Dar es Salaam asilimia 9.4, Dodoma asilimia 7 na Kagera asilimia 6.7. Mikoa yenye viwango vya chini ni Simiyu asilimia 1.1, Njombe asilimia 1.2 na Lindi asilimia 1.5.

Kwa upande wa makosa, wizi unaongoza kwa asilimia 18.2, ukifuatiwa na kuingia nchini bila kibali asilimia 11.2 na ubakaji asilimia 7.4. Makosa yenye idadi ndogo ni rushwa asilimia 0.01, uharamia asilimia 0.03 na utakatishaji fedha asilimia 0.03.

Kazulaya amesema takwimu hizo ni nyenzo muhimu kwa watunga sera, akibainisha kuwa zinaonyesha maeneo yanayohitaji uamuzi wa haraka, mfano ongezeko la kesi za wizi.

Amesema mwaka 2025, magereza yalipokea jumla ya wahalifu 128,395 kutoka mahakama mbalimbali, wakiwemo wafungwa 27,396 na mahabusu 100,969. Mwaka 2024 walikuwa 121,768, ambapo wafungwa walikuwa 27,512 na mahabusu 94,296.

Hapa, idadi ya wafungwa waliopokelewa ilipungua kwa asilimia 0.4 huku mahabusu wakiongezeka kwa asilimia 7.

Aidha, amesema baadhi ya wahalifu wamekuwa wakihamishwa kutoka gereza moja kwenda jingine kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matibabu, mafunzo na usikilizwaji wa kesi zao.

Katika juhudi za urekebishaji, wafungwa wanaendelea kupewa mafunzo ya ufundi stadi, takwimu zinaonyesha mwaka 2025 wafungwa 11,400 na mahabusu 1,938 walipatiwa mafunzo hayo, ikilinganishwa na wafungwa 11,049 na mahabusu 1,913 mwaka 2024.

Hii ni ongezeko la asilimia 3.1 kwa wafungwa na asilimia 1.3 kwa mahabusu.

Kazulaya pia ameeleza kuwepo kwa kundi la wahalifu wanaorudia makosa na kurejea magerezani, akisema serikali inaendelea kufanya tafiti kubaini chanzo na namna ya kupunguza hali hiyo.

Ametoa wito kwa jamii kutoa elimu juu ya madhara ya uhalifu kuanzia ngazi ya familia, shule na taasisi za dini ili kuzuia kizazi kipya kuingia kwenye uhalifu.

Kwa upande wake, Meneja wa Utafiti na Ubunifu na Viwango kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mariam Kitembe amesema takwimu ni nyenzo muhimu katika mipango ya maendeleo na kusisitiza umuhimu wa kuziboreshwa kila mwaka.

“Takwimu za mwaka 2025 hazitishi, lakini tunahitaji za mwaka 2026 ili kulinganisha na kuona chanzo cha kupungua kwa mahabusu na kuongezeka kwa wafungwa,” amesema.

Naye, Kamishna wa Fedha na Mipango, Chacha Jackson amesema takwimu hizo zina umuhimu mpana hata kwa taasisi nyingine na zinaonyesha mageuzi ya mfumo wa magereza kutoka adhabu kwenda urekebishaji.

Kwa upande wake, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Nicodemus Tenga kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba ya mgeni rasmi, amesisitiza kuwa takwimu za magereza zinaisaidia serikali kupanga sera, kufanya uamuzi sahihi na kuboresha mfumo wa haki jinai kitaifa na kimataifa.

Amesema msisitizo wa viongozi wakuu wa nchi katika matumizi ya takwimu unalenga kuhakikisha maamuzi yote yanafanywa kwa ushahidi na uhalisia wa takwimu na kusaidia kuwepo kwa uwajibikaji.

“Takwimu hizi sio za kwanza ni za 14 na zinaendelea kuboreshwa kila mwaka unaendana na mahitaji ya takwimu husika,” amesema Tenga.

Amesema ripoti hiyo inasaidia idara mbalimbali katika kubadili changamoto za wafungwa na kuweza kusaida kutungwa kwa sera na kujua mapungufu ya haki jinai.