Dar/Arusha. Jitihada za wadaiwa wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited zimegonga ukuta baada ya Mahakama ya Rufani kukataa kusikiliza rufaa yao ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliowaamuru kuilipa kampuni hiyo zaidi ya Sh68 bilioni wanazodaiwa.
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Barke Sehel (kiongozi wa jopo), Sam Rumanyika na Mustafa Ismail, baada ya kubaini kasoro ya ukiukwaji wa sheria usiorekebishika katika rufaa hiyo ya madai namba 804 ya mwaka 2023.
Kasoro hiyo ni uamuzi wa warufani, ambao walikuwa makundi mawili tofauti yaliyowasilisha notisi mbili tofauti za rufaa kila kundi notisi yake kwa nyakati tofauti kujiunganisha wenyewe katika hati moja ya sababu za rufaa (hati ya rufaa), badala ya kuwasilisha hati mbili za rufaa.
Rufaa hiyo ilikatwa na kampuni za SGS Societe Generale De Surveillance S.A, SGS Tanzania Superintendence Company Limited, Craig John Wilson, Samuel Kojo Gyan, Jean Fredrick Georges Marie Hellen, Denise F. De Geyseller, Kwok Wang Ng na Jean Paul Antoine Bonvin.
Warufani hao walikata rufaa hiyo dhidi ya kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa jijini Dar es Salaam, James Rugemalira.
Katika uamuzi huo ulioandikwa na Jaji Ismail kwa niaba ya jopo, uliotolewa Machi 18, 2026, mahakama hiyo imesema ukiukwaji huo wa sheria uliofanywa na warufani katika rufaa hiyo ni kosa kubwa na la msingi lisiloweza kuokoa rufaa yao.
“Kwa kweli, linaifanya rufaa kuwa dhaifu na batili, na hakuna kiwango chochote cha matumizi ya kanuni ya overriding objective (kanuni ya mahakama kupuuza makosa madogo hasa ya kiufundi) kinachoweza kuihuisha,” amesema Jaji Ismail baada ya kuchambua sheria na hoja za pande zote na kusisitiza:
“Kwa sababu ya kasoro hiyo, tunaamua kuwa rufaa hii haina uhalali na kwa hivyo tunaifuta kwa gharama.”
Rufaa hiyo inajengwa na historia ya kesi iliyochukua takribani miaka 26 mpaka sasa.
Mwaka 2000, VIP Engineering ilifungua kesi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, dhidi ya kampuni za SGS Societe na SGS Tanzania pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kesi ya kibiashara namba 16/2000.
VIP Engineering ilizilalamikia kampuni hizo kufanya uzembe na/au udanganyifu katika utoaji wa ukaguzi uliothibitisha kuwa mzigo wa tani 3,000 za mchele iliouagiza kutoka kampuni ya Messrs Orco International Pte Limited ya Singapore ulikidhi masharti ya mkataba.
Ilidai hakukuwa na ukaguzi wowote uliofanyika na kwamba mchele huo ulikuwa na ubora duni na kiasi pungufu, jambo lililoisababisha hasara kubwa sana.
Wakati huo SGS Societe ilikuwa na mkataba na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kufanya ukaguzi wa lazima wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuingizwa nchini Tanzania, pamoja na kampuni yake tanzu ya SGS Tanzania.
Katika hukumu iliyotolewa Desemba 19, 2005, Mahakama iliziona SGS Societe na SGS Tanzania kuwa na kosa, kwamba zilikiuka wajibu wa uangalizi waliokuwa nao kwa mdai, VIP Engineering.
Hivyo, iliziamuru kuilipa VIP Engineering fidia ya hasara maalum ya dola za Marekani 650,350.08; zaidi ya Sh1.665 bilioni kwa kiwango cha ubadilishaji fedha cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) cha Machi 27, 2026 (Sh2,561.6832 kwa dola).
Pia waliamuriwa kuilipa fidia ya hasara ya faida na hasara ya kiuchumi ya dola za Marekani 6,000,000.00 (zaidi ya Sh15.37 bilioni kwa sasa), ada za mahakama kiasi cha Sh22,000,000, riba ya asilimia 20 kuanzia Mei 15, 1999 hadi tarehe ya hukumu, pamoja na gharama za kesi.
Hata hivyo, utekelezaji wa amri hiyo haukufanyika hadi mwaka 2021, miaka 20 baadaye, ambapo VIP Engineering ilifungua shauri la maombi mengine yaliyolenga kufanikisha utekelezaji wa hukumu hiyo.
Katika maombi hayo ya kibiashara Na. 169 ya 2021, VIP Engineering iliiomba mahakama iamuru utekelezaji wa hukumu dhidi ya wakurugenzi na maafisa wakuu wa wadaiwa badala ya kampuni.
Mahakama hiyo, katika uamuzi wake wa Februari 28, 2022, ilikubali ombi hilo.
Hivyo, ilielekeza kuwa hukumu itekelezwe dhidi ya Benedict K. Karuho, Harry Leonard Freake, Andrew Siggy Collins pamoja na warufani wa tatu hadi wa nane (waliotajwa kwenye rufaa hii), ambao wakati huo walikuwa wakurugenzi, mameneja na maafisa wakuu wa wadaiwa.
Mwaka mmoja baadaye, Machi 17, 2023, zilitolewa hati sita za kuwakamata na kuwafunga warufani wa tatu hadi wa nane kwa muda wa miezi sita kwa kushindwa kulipa deni la hukumu hiyo.
Aprili 6, 2023, warufani wa tatu hadi wa nane waliwasilisha notisi ya kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi huo, huku warufaniwa katika rufaa hiyo tarajiwa wakiwa ni SGS Societe, SGS Tanzania na VIP Engineering.
Aprili 13, 2023, SGS Societe na SGS Tanzania nao waliwasilisha notisi ya rufaa kupinga hati hizo za ukamatwaji, huku warufani wa tatu hadi wa nane wakiwa ni warufaniwa pamoja na VIP Engineering.
Desemba 22, 2023, makundi hayo mawili ya warufani yaliwasilisha hati ya rufaa ya pamoja badala ya hati mbili sawa na idadi ya notisi.
Hati hiyo iliwaunganisha warufani wa kwanza na wa pili SGS Societe na SGS Tanzania, ambao awali walikuwa warufaniwa pamoja na warufani wa tatu hadi wa nane dhidi ya VIP Engineering.
Kutokana na tofauti hiyo, siku iliyopangwa kusikilizwa rufaa hiyo, kwanza Mahakama iliwataka mawakili wa pande zote kutoa hoja kuhusu uhalali na ufasaha wa rufaa hiyo.
Wakili wa warufani wote, Timon Vitalis, alikiri kuwa rufaa ina mapungufu.
Alieleza kuwa kwa kanuni ya 88(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka 2009, notisi halali ya rufaa ni moja tu inayowasilishwa kwanza, na kunapokuwepo notisi zaidi ya moja, nyingine zinazofuata huchukuliwa kuwa notisi za anuani ya huduma kwa wahusika.
Hivyo, Wakili Vitalis alibainisha kuwa notisi halisi ni ile iliyowasilishwa awali na warufani wa tatu hadi wa nane.
Hata hivyo, alidai kuwa upungufu huo unaweza kurekebishwa kwa kutumia kanuni ya overriding objective chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, Sura ya 141 (AJA).
Aliomba Mahakama, ikiona haja ya marekebisho, iruhusu warufani kuwasilisha hati mbili tofauti za rufaa kwa mujibu wa kanuni ya 111 na kanuni ya 4(2)(a) na (b) za Kanuni za Mahakama.
Wakili wa mrufaniwa, Respicius Didace, alieleza kuwa warufani kuwasilisha hati moja ya rufaa wakati kuna notisi mbili za rufaa, bila amri ya mahakama kuziunganisha, huku warufani katika notisi ya pili wakiwa warufani katika hati ya rufaa badala ya kuwa warufaniwa, ni kinyume cha kanuni ya 88(1).
Alisisitiza kuwa kutofuata sharti hilo ni kosa lisilorekebishika kwa kutumia kanuni ya overriding objective pale masharti ya lazima ya kitaratibu yanapokiukwa, na kwamba hati ya rufaa hiyo si halali; suluhisho pekee ni kuifuta.
Mahakama imesema kanuni ya 111 inaipa mamlaka ya kuruhusu marekebisho ya sehemu yoyote ya kumbukumbu ya rufaa kwa makosa madogo tu, si makosa ya msingi ya kitaratibu.
Pia imesema kuwa si kila kasoro katika kumbukumbu ya rufaa inaweza kurekebishwa kwa kutumia kanuni ya overriding objective, isipokuwa kasoro za kiufundi tu.
“Kanuni ya overriding objective siyo kama mungu wa kale wa Kigiriki aitwaye Panacea anayetoa tiba kwa kila tatizo; haikusudiwi kurekebisha kila aina ya kasoro na upungufu unaofanywa na wahusika mahakamani,” amesema Jaji Ismail.
“Kanuni ya overriding objective haiwezi kutumika kwa kupuuza masharti ya lazima ya sheria ya utaratibu yanayogusa msingi wa shauri.”
Hivyo, mahakama imesema kuwa kwa maoni yao, kanuni ya 88(1) inaweka sharti la lazima la kitaratibu linalogusa msingi wa mwenendo wa rufaa, si suala la kiufundi tu linaloweza kurekebishwa kwa urahisi kwa kutumia kanuni ya overriding objective, bali linahitaji hatua kali za kulitupilia mbali.
