Mtwara. Mbinu ya kujifanya bubu ili kuomba misaada kutoka kwa taasisi na wananchi imemponza kijana mmoja baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Mtwara akiwa na Sh1.8 milioni alizodaiwa kukusanya kwa njia ya udanganyifu.
Mtuhumiwa huyo, Ibrahim Nzumbi Mugendi (31), mkazi wa mkoa wa Kigoma, anadaiwa kujifanya ana tatizo la kuongea ili kuomba michango kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali, kabla ya kufichuliwa na kukamatwa na polisi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Machi 27, 2026, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara,Issa Suleiman amesema mtuhumiwa aliwasili mkoani humo Februari 18, 2026 na kufikia katika moja ya nyumba za kulala wageni.
Kamanda Suleiman amesema siku chache baadaye, Februari 26, mtuhumiwa alifika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kuomba kibali cha kuchangisha fedha, akidai anahitaji msaada kutokana na changamoto ya kiafya inayomfanya ashindwe kuongea.
“Baada ya kupewa kibali hicho, alianza kutembelea taasisi mbalimbali za serikali pamoja na watu binafsi akiomba michango kwa madai ya kusaidiwa kutokana na hali yake ya kiafya,” amesema.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kamanda huyo, uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa mtuhumiwa hakuwa na tatizo lolote la kuongea, bali alitumia mbinu ya kujifanya bubu ili kujipatia fedha kutoka kwa wananchi wenye huruma.
Amesema mtuhumiwa alikamatwa Machi 25, 2026 akiwa na jumla ya Sh1.8 milioni, fedha ambazo alidaiwa kukusanya kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali ndani ya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa polisi, mtuhumiwa alifanikiwa kufika katika ofisi za taasisi 10 za serikali pamoja na watu binafsikabla ya kufichuliwa na kukamatwa.
“Baada ya kupata taarifa na kufanyika kwa uchunguzi wa kina, tulibaini kuwa mtu huyo hana tatizo lolote la kuongea. Ndipo tukamkamata na kumhoji zaidi kuhusu fedha alizokusanya,” amesema Kamanda Suleiman.
Ameongeza kuwa upelelezi wa shauri hilo unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara tu uchunguzi utakapokamilika ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limewataka wananchi kuwa makini na watu wanaotumia mbinu mbalimbali za kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.
Kamanda Suleiman amesema matapeli wamekuwa wakibuni njia tofauti za kuwahadaa wananchi, akiwataka watu kuthibitisha taarifa za watu wanaoomba michango kabla ya kutoa fedha.
“Tunawasihi wananchi kuwa makini na matukio ya aina hii. Ni muhimu kuthibitisha taarifa au vibali vya watu wanaoomba michango ili kuepuka kudanganywa,” amesema Kamanda Suleiman.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wote wanaojihusisha na vitendo vya utapeli vinavyolenga kuwaumiza wananchi.