May Day itatue matatizo ya wastaafu, si ya wafanyakazi pekee!

Kutokana na maumivu na malalamiko mengi aliyopokea mstaafu wetu kutoka kwa wastaafu wenzake juu ya makala ya Ijumaa iliyopita kuhusu mikopo wanayolipiwa na kukopeshwa juu kwa juu na hizi benki za dotcom zinazodai kufanya kile kiitwacho ni ‘kumsaidia mstaafu’, inavyowatesa wastaafu!

Mstaafu anaona kuna njia tatu kwa Serikali na vibubu husika zinazopaswa kuchukuliwa fasta, ili kuwaokoa wastaafu hawa walioijenga, kuipigania na kuilinda nchi kwa jasho na damu yao, hadi kuifikisha hapa pa watu kulipana shilingi milioni kumi na nne na ushee kwa mwezi, huku mstaafu aliyelijenga Taifa akiishia kulipwa pensheni ya shilingi laki mbili unusu kwa mwezi! Kweli, binadamu wote ni sawa?

Siri-kali na vibubu hivi vitakuwa vimefanya jambo la maana sana kwa kutangaza hatua hizo, hususan siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day), ili pamoja na mengine mengi, kuwapa moyo wastaafu watarajiwa ambao wengine wana kawaida ya kujidanganya kuwa hawatazeeka na kustaafu, potelea mbali kwamba kikokotoo kinakula nao sahani moja!

Moja, kibubu husika cha akiba ya wafanyakazi na Serikali vifanye haraka kuanzisha benki ndogo ya kuwasaidia wastaafu kikwelikweli, si kwa haya maneno ya kanga, kupata mikopo midogo midogo yenye marejesho na riba nafuu zinazoeleweka kwa wastaafu, si hizi riba zinazomfanya mstaafu apate shilingi laki moja sitini badala ya laki mbili na hamsini elfu baada ya riba na marejesho kuchukua chao!

Siri-kali ihimize kibubu kuanzisha benki ndogo ya wastaafu kwa ajili ya kuwapa mikopo midogomidogo ya kuwawezesha hata kununua vimashine vya kupimia kisukari na vya kupimia BP yao, maana ndio magonjwa yanashika bango mstaafu anapostaafu, na Serikali imeshawahi kusema haiwezi kutoa matibabu ya bure kwa wazee… lakini unaweza kununua ma V8 kwa waheshimiwa wake!

Mbili. Pensheni ya mstaafu wa kima cha chini, kama si cha chizi, iongezwe haraka siku ya May Day kutoka shilingi laki mbili na elfu hamsini anazopata kwa mwezi, na kuwa shilingi laki tano kwa mwezi. Inawezekana. Ni utashi tu, kama tuliokuwa nao wakati tunajenga nchi hii!

Kama nchi imefika mahali pa kumlipa asemekanaye kuwa ni mwakilishi wa wananchi, wakiwemo wastaafu, shilingi milioni 14 na ushee kwa mwezi, inaweza pia kumlipa mstaafu aliyeijenga nchi shilingi laki tano kwa mwezi. Rudia, ni utashi tu.

Ni utashi tu utakaowezesha wawakilishi wale wapokee shilingi milioni kumi tu kwa mwezi (na bado ni nyingi kwa nchi maskini kama hii!) ili nne na ushee zilizobaki zikaongeze pensheni ya mwezi ya mstaafu wa kima cha chini aliyeijenga nchi hii wakati wawakilishi wengi bado wako shule za vidudu!

Mwakilishi atakayekosa utashi na kuona milioni kumi ni ndogo kwake, atakiwe kuchapa lapa akalime na awaachie wengine wenye utashi na wanaoweza kukubali kugawana na wastaafu keki ya taifa ambayo hadi sasa, baada ya miaka 65 ya Uhuru, yeye aliyeshiriki kwa utashi wake ‘kuipika’ keki ya taifa anaambulia harufu tu, huku akiishia kuangalia wenye meno wakiitafuna keki, na si wenye moyo akina wastaafu wa kima cha chizi!

Tatu. Siri-kali na vibubu husika viandae utaratibu fasta wa kumpa mstaafu wa kima cha chini shilingi milioni tano na laki tano walizomuahidi kumpa… atakapokuwa mkazi wa Kinondoni, na si akiwa hai! Acha kwanza nicheke kwa uchungu! Milioni tano laki tano kwa maiti? Acheni mizaha na maisha ya watu!

Unampa mstaafu shilingi milioni tano na laki tano ulizoahidi kumpa mara tu anapokuwa mkazi wa Kinondoni, na si akiwa hai? Yaani una jeuri kabisa ya kutamba kwa matangazo magazetini kuwa utatoa shilingi milioni tano na laki tano kwa mstaafu akiwa maiti! Acheni uchuro. Wale wazee wakulima waliolilisha taifa wakati tunalijenga, wao wakifariki watapewa shilingi ngapi?

Rudia, nacheka kwa uchungu ninapokumbuka yatokeayo kwenye jamii zetu. Mstaafu anaumwa na ndugu zake wanashindwa hata kwenda kumjulia hali tu, lakini mara anapokuwa mkazi wa Kinondoni ndugu zake hao hushindana kumnunulia suti ya kumpeleka Kinondoni, wakati mara ya mwisho kumnunulia suti ya mtumba ilikuwa wakati anastaafu miaka 17 iliyopita!

Inasikitisha sana kuona kibubu kikifanya yale yale yanayofanywa na jamii— jeneza la bei mbaya, maua ya gharama na ‘video’, kama aimbavyo nguli wetu mmoja… kwa kumpa mstaafu shilingi milioni tano na laki tano akiwa tayari mkazi wa Kinondoni na si akiwa hai, ambapo ataweza kujinunulia dawa za maradhi yake ya uzee, huku Serikali ikisema haiwezi kumpa matibabu ya bure! Mpeni mstaafu shilingi milioni tano laki tano mlizoahidi akiwa hai, atajua mwenyewe afanye nini!

Acheni kucheza na maisha ya wastaafu, waheshimiwa. Fanyieni kazi haraka haya muyatangaze siku ya Wafanyakazi, ambao wote ni wastaafu watarajiwa! Wastaafu wanasema, si lazima mpaka wawe “Gen Old”!

0754 340606 / 0784 340606