Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abubakari Asenga, ametoa pole kwa wananchi wa jimbo hilo waliokumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro.
Akizungumza leo Machi 27, 2026 katika Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia maafa, Mara baada ya kupokea msaada wa magodoro, mablanketi na chakula, Asenga amesema kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha wananchi waliopata madhara wanapata msaada wa haraka ili kupunguza athari walizokumbana nazo.
Mbunge huyo ameeleza shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya dharura kwa ajili ya kuwasaidia waathirika.
Amesema kuwa tayari wamepokea msaada unaojumuisha magodoro 75, mablanketi pamoja na tani 10 za mahindi, ambavyo vitasambazwa kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo wakati wakisubiri hatua zaidi za msaada kutoka serikalini.
Aidha, Asenga amewapongeza wananchi pamoja na kamati ya maafa ya wilaya kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa juhudi kubwa walizozifanya kuokoa maisha ya watu. Amebainisha kuwa hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya vifo iliyothibitishwa licha ya uharibifu mkubwa wa makazi ya wananchi.
Ameongeza kuwa baada ya kupokea taarifa za kuwepo kwa wananchi wasio na mahali pa kulala, ofisi yake ilichukua hatua za haraka kutafuta msaada wa magodoro, mablanketi pamoja na chakula ili kuhakikisha mahitaji muhimu yanapatikana kwa wakati.
Kwa upande mwingine, amesema ofisi ya mbunge imefanikiwa pia kupata unga ambao unatarajiwa kusambazwa kesho Jumamosi katika maeneo yaliyoathirika zaidi ikiwemo Ifakara, Lumemo na Michenga, ili kuwafariji na kuwasaidia wananchi waliokumbwa na adha hiyo.
Asenga amesisitiza kuwa wataendelea kuisimamia serikali kuhakikisha inatekeleza mipango ya kudhibiti athari za mafuriko, ikiwemo kufufua mabwawa, kupanua mito pamoja na kujenga miundombinu ya kinga kama matuta ili kupunguza madhara ya mafuriko siku zijazo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, takribani kaya 100 zenye jumla ya watu wapatao 500 zimeathirika na mafuriko hayo. Ingawa baadhi ya maeneo yameanza kupungua maji na wananchi kurejea makwao, bado wapo ambao hawajaweza kurudi kutokana na kiwango kikubwa cha maji kilichoingia kwenye makazi yao.
Kwa ujumla, juhudi za serikali zinaendelea kusaidia waathirika wa mafuriko katika Jimbo la Kilombero, huku msisitizo ukiwa ni kuhakikisha misaada ya dharura inawafikia wananchi wote walioathirika na kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti majanga kama haya siku zijazo.

