……..
MKAZI wa Mtaa wa Ocean Road jijini Dar es Salaam, Hamid Ahmed Hussein, amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na jumla ya mashtaka 43, yakiwemo ya Uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.
Mashtaka hayo yaliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi Franco Kiswaga, Hamid Ahmed Hussein anadaiwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kughushi nyaraka za uongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Wakili wa Serikali Cathbet Bilinyi amedai kuwa Humid Ahmed Hussein mbali na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pia atuhumiwa kwa kutumia ulaghai wake na kujipatia fedha katika kampuni mbalimbali zikiwemo zilizopo katika Wilaya ya Temeke na Mikocheni Jijini Dar es Salaam.
Upande wa mashtaka ulieleza kuwa kati ya Januari 2020 na Februari 2026, mtuhumiwa alighushi stakabadhi na hati za malipo akidai zimetolewa na Manispaa ya Temeke, ilhali si halali, na kupitia mbinu hiyo alijipatia fedha kutoka kampuni binafsi, kiasi kinachodaiwa kufikia hadi Sh. bilioni tano.
Aidha, katika shtaka la utakatishaji fedha, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alifanya miamala ya kifedha kwa lengo la kuficha asili ya fedha zinazodaiwa kupatikana kwa njia haramu.
Hakimu Kiswaga amesema kosa la utakatishaji fedha halina dhamana na mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo katika hatua ya sasa.
Kwa upande wa utetezi, wakili Josephat Mabula aliomba mahakama izingatie haki ya mtuhumiwa, akieleza kuwa amekaa mahabusu kwa siku 23 tangu kukamatwa kwake.
Mahakama imeelekeza upelelezi ukamilishwe haraka, huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Aprili 9, 2026 kwa ajili ya kutajwa tena.
Aidha wakitoa maoni yao kutokana na kesi hiyo, baadhi ya wananchi wa Jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuwa makini na raia wa kigeni kama hao kwa kuwa wanakosa uaminifu huku wakisababisha usumbufu kwa Taifa.
Mwisho