Tanzania yapanda viwango vya CAF, yaipiku Tunisia

Tanzania imepanda kwa nafasi moja katika chati ya viwango vya ubora vya nchi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kulingana na mafanikio ya klabu kwenye mashindano ya Afrika.

Chati hiyo inatokana na tathmini ya ushiriki wa miaka mitano wa klabu za nchi husika katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Tanzania ambayo ilikuwa nafasi ya sita, sasa ipo nafasi ya tano huku Tunisia iliyokuwa nafasi ya tano ikishuka hadi ya sita.

Kupanda kwa Tanzania kumetokana na kukusanya idadi ya pointi 82.5 katika kipindi cha misimu mitano iliyopita ya ushiriki wa klabu zake katika mashindano ya klabu Afrika.

Idadi kubwa ya pointi kwa Tanzania imekusanya msimu uliopita ambao imekusanya jumla ya pointi 30.

Pointi 20 imezipata kutokana na Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na pointi 10 imevuna kwa Yanga kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika msimu wa 2023/2024, Tanzania ilikusanya idadi ya pointi 24 na msimu wa 2022/2023 ilikusanya pointi 21.

CA 01

Chati hiyo inaongozwa na Misri ambayo ina pointi 190.5, huku nafasi ya pili ikiwa Morocco yenye pointi 142.

Nafasi ya tatu ipo Afrika Kusini ambayo ina pointi 131 na Algeria inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 130.

Chati hiyo ya Caf ya ubora wa hupangwa kwa kuzingatia pointi ambazo klabu zimekusanya katika ushiriki wa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kwa kipindi cha misimu mitano ya nyuma.

Timu huanza kuhesabiwa pointi hizo kuanzia hatua ya makundi hadi ile ya fainali na zinazotolewa katika raundi ya kwanza na ya pili hazipati pointi yoyote.

Kwa mujibu wa muongozo wa sasa, ushiriki wa kuanzia hatua ya makundi hadi fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika unakuwa na idadi kubwa ya pointi kulinganisha na ushiriki wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, bingwa anapata pointi sita (6), mshindi wa pili anapata pointi tano (5), timu mbili zinazoishia nusu fainali kila moja inapata pointi nne, pointi tatu ni kwa timu inayotolewa katika robo fainali, timu inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi inapata pointi mbili na pointi moja hupata timu ambayo inashika mkia kwenye kundi.

Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika,timu ambayo inashika mkia kwenye kundi inapata pointi 0.5, timu inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi inapata pointi moja (1), pointi mbili (2) ni kwa timu inayotolewa katika robo fainali,  timu mbili zinazoishia nusu fainali kila moja inapata pointi tatu (3), mshindi wa pili anapata pointi nne (4) na  bingwa anapata pointi tano (5).

Kisha pointi hizo zinazidishwa kwa alama ya msimu mmommoja katika mitano iliyopita ambao msimu wa tano nyuma unakuwa ni alama moja, msimu wa nne unakuwa ni alama mbili, msimu wa tatu unakuwa ni alama tatu, msimu wa pili nyuma unakuwa ni alama nne na msimu mmoja nyuma unakuwa ni alama tano.