Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini James Bwana amesema wanafuatilia kwa ukaribu tukio la kijana aliyedaiwa ni Mtanzania ambaye ameonekana akipigwa nchini humo huku akilazimishwa kufunga duka lake.
Kupitia video fupi iliyotumwa mtandaoni kijana huyo wa kiume akiwa kwenye duka lake,alitakiwa kuonyesha nyaraka ambazo alizionyesha akitamka neno ‘valid’ikiwa na mana ziko sawa’
Hata hivyo alianza kutandikwa viboko sehemu za juu ya mwili wake akitakiwa kufunga duka lake.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo leo Machi 27, 2026 Balozi Bwana amesema kama kuna mtu mwneye taarifa ya kijana huyo na mahali alipo wafanye mawasiliano ili kubaini kilichotokea.
“Tumeiona video japo ni ngumu kufahamu kama huyo ni Mtanzania kwa kuangalia, kwahiyo tunafuatilia kujua kama ni kweli huyo ni Mtanzania mwenzetu na sio video ya kutengeneza Ai,
“Kama kuna mtu anamfahamu anaweza kutusaidia kwa haraka ni wapi alipo na mawasiliano yake,”amesema.
Balozi Bwana amesema zipo oparesheni zinaendelea huko Afrika kusini kudhibiti wahamiaji haramu akiwataka Watanzania wanaokwenda nchi za watu kuhakikisha wanafuata utaratibu.
Amesema wapo baadhi ya watu hukimbilia mataifa hayo kupitia njia za panya na kuishi wanavyoishi, yanapotokea matatizo huwakumba kutokana na utaratibu mbovu waliotumia kuingia nchi hizo.
Balozi Bwana amesema wapo raia kutoka mataifa mbalimbali wanaopitia changamoto Afrika kusini na mataifa mengine kutokana na matatizo yao ya kutofuata utaratibu wa uhamiaji.
“Kama ataondoshwa nchini ni moja hakuwa na vibali vya kuishi huko na hana vibali halali vya kuonyesha kuwa yupo kihalali inakuwa ni ngumu kuingilia maana inakuwa ni utaratinu wa uhamiaji na huo upo mataifa mengi tu,”amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi